RC Wangabo aililia MV Lyemba kuhudumia wananchi ziwa Tanganyika
Mwambawahabari
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.
Joachim Wangabo ameishauri Mamlaka ya Bandari nchini kuona umuhimu wa kuifufua
MV Lyemba ambayo ilikuwa ikitoa huduma ya kubeba mizigo na abiria katika ziwa
Tanganyika ambapo kwa sasa hakuna hata meli moja inayotoa huduma ya kubeba
abiria katika ziwa hilo linalounganisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma na
nchi za jirani ikiwemo Zambia pamoja na Jamhuri ya Demokrasia ya watu wa Congo.
Mh. Wangabo amesema kuwa
hali ya usafiri katika ziwa tangayika sio nzuri ni mbaya kutokana na wananchi
kupanda majahazi, mitumbwi na bodi ambapo mara kadhaa wamekuwa wakijazana jambo
ambalo ni hatari kwa usalama wa Maisha ya wananchi hao.
“Hili jambo hili Mamlaka ya
Bandari pamoja na vyombo vuingine vinavyohusika mfanye haraka sana kwakweli ile
meli ya MV Lyemba kwakweli ni mkombozi katika hili ziwa Tanganyika kwasababu
hakuna chombo kingine kikubwa mbacho kinaweza kikasaidia hawa wananchi pamoja
na mizigo yao watu wanahangaika sana na ni miaka sasa imekuwa ni muda mrefu,
miaka kadhaa imekwishapita kwahiyo hili mlipaswa mlione hata kwa jicho la
huruma basi,” Alisema
Na kuonya kuwa isifike hatua
watu wakapoteza Maisha kwenye Ziwa Tanganyika ndipo ije kuonekana kuna umuhimu
wa kuokoa Maisha ya watu wakati wamekwishaangamia na kuwataka wachukulie jambo
hilo kwa uzito mkubwa kabla ya kupoteza maisha ya watu wanaoishi katika mwambao
wa ziwa hilo.
Mh.Wangabo ameyasema hayo
alipofanya ziara katika Tarafa ya Kasanga kujionea maendeleo ya ujenzi wa barabara
yenye urefu wa km 107 kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga ambapo imekamilika
kwa asilimia 97 pamoja na bandari ya Kasanga ambayo imekamilika kwa asilimia 50
akiwa pamoja na wajumbe wa kamati ya usalama ya mkoa pamoja na wataalamu kutoka
Mamlaka ya Bandari pamoja na Wakala wa wa Barabara nchini.
Aidha, akitoa taarifa kwa
niaba ya Meneja wa Badari hizo za Ziwa Tanganyika Yudas Suwanyi alisema kuwa
kuna meli kadhaa zinazohudumu katika ziwa hilo ambazo hubeba mizigo peke yake ikiwemo
meli ya MV malagalasi inayomilikiwa na Mtanzania inayofanya safari zake
kutegemeana na upatikanaji wa mizigo katika mikoa hiyo.
Wakati akitoa taarifa ya
uboreshaji wa bandari hiyo ya Kasanga kaimu mhandisi wa bandari za ziwa
Tanganyika Nyakato Lwamnana amesema kuwa pamoja na maboresho ya majengo kadhaa
ikiwemo nyumba za watumishi, jengo la kusubiria abiria, maghala, ofisi kadhaa
pia kuna upanuzi wa gati unafanyika ambapo kwa sasa kuna gati la urefu wa mita
20 lenye uwezo wa kupokea meli moja na kupanuliwa hadi kuwa na urefu wa mita
120 na kuweza kuchukua meli mbili kwa wakati mmoja ili kuepuka changamoto ya
kusubiriana.
“Gharama za mradi ni 4,000,764,000/=,
ambapo ulianza tarehe 29.4.2019 mradi ni wa mwaka mmoja mpaka tarehe 28.4.2020
tunategemea mradi huu kukamilika kwasasa umefikia asilimia 50 na muda ambao
umekwishapita ni asilimia 76 kama mnavyoona muda mrefu umepita kuliko
utekelezaji utekelezaji tuko asilimia 50,” Alisema.
Kwa upande wake meneja wa
Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) mkoani Rukwa Mhandisi Masuka Mkina alisema
kuwa imebaki changamoto ndogo ya kupotomoka kwa udongo (landaslide) ili kuweza
kukamilisha barabara hiyo iliyoanza kujengwa tarehe 13.1.2010 ambapo hadi
kufikia tarehe 31.12.2019 ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 97 na kwa bajeti ya
mwaka 2019/2020 serikali imetenga shilingi bilioni 5.8 kumalizia ujenzi huo
unaotarajiwa kumalizika mwezi June, 2020.
“Wanampango wa kumleta
mtaalamu kusudi aweze kufanya upembuzi wa eneo hili halafu awape muongozo wa
nini kifanyike, namna ya kujenga eneo hili ambalo udongo umeporomoka, wamesema
wameshampata Kampuni ya Noro Plan Tanzania ndio mshauri ambae atakuja kufanya
utafiti hapa kujua chanzo na nini cha kufanya,” Alieleza.
Katika ziara hiyo Mh.
Wangabo na timu yake pamoja Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Rukwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa Ndg.
Enos Budodi waliridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuwataka wananchi
kutumia fursa zinazopatika kutokana na kukamilika kwa miradi hiyo ya kimkakati
ya mkoa.
Post a Comment