NAIBU WAZIRI IKUPA AHIMIZA VYAMA VYA WATU WENYE ULEMAVU KUSHIRIKIANA NA SERIKALI
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa akizungumza na viongozi wa Mkoa na Vyama vya Watu wenye Ulemavu wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Dodoma. (Kushoto) ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Mjini Bw. Edward Mpogolo (Kulia) ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Felisiana Mboya
Mwamba wa habari
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ameviasa Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuendeleza ustawi wa Watu wenye Ulemavu.
Naibu Waziri Ikupa ameyasema
hayo alipofanya ziara Mkoani Dodoma kukagua utekelezaji wa masuala
ya Watu wenye Ulemavu ndani ya mkoa huo, ambapo alikutana na viongozi Mkoa na Vyama
vya Watu wenye Ulemavu.
Mhe. Ikupa alieleza kuwa ushirikiano
baina ya Serikali na vyama vya watu wenye ulemavu ni muhimu katika kuhakisha haki
na masilahi ya watu wenye ulemavu yanalidwa kwa kuzingatia Sera, Sheria na
Miongozo mbalimbali.
“Serikali imeendelea kuchukua
hatua na kutekeleza jukumu lake la kuhamasisha na kuwalinda watu wenye ulemavu
nchini kwa kuhakikisha haki za kundi hilo maalumu zinatekelezwa,” alisema Ikupa
Aidha, alisisitiza uongozi
wa Mkoa kuhakikisha unahusisha mahitaji maalumu ya wenye ulemavu katika bajeti
wanazozitenga, kutoa elimu na taarifa juu ya upatikanaji wa dawa, mafuta ya
watu wenye ualbino na vifaa saidizi, na uundwaji wa kamati za kuhudumia wenye
ulemavu.
Aliongezea kuwa, ni vyema
Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na maafisa ustawi wa jamii wakahakikisha
wanawasaidia watu wenye ulemavu wanapokabiliana na changamoto kwenye uandikaji
wa maandiko ya kuomba mikopo.
“Unakuta kikundi cha watu
wenye ulemavu wanakuwa wabunifu na wanawazo zuri la kuanzisha mradi au biashara
lakini wanakumbana na changamoto ya kuaandaa andiko la miradi yao na hivyo
kuwafanya wakate tamaa mapema,” alisema Ikupa
Pia, aliwasii Maafisa Ustawi
wa Jamii kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu wenye ulemavu na kuendelea
kuweka mifumo mizuri ya kutunza taarifa hizo.
Kwa upande wake Katibu
Tawala wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Bw. Edward Mpogolo aliunga mkono na kuyapokea
maelekezo yote ya Naibu Waziri na kumhakikishia kuwa Mkoa wa Dodoma utakuwa
mstari wa mbele katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa.
“Tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Vyama
vya Watu wenye Ulemavu ili kuangalia namna bora ya kuwahudumia kwa kuzingatia
mahitaji yao,” alisema Mpogolo.
Naye Katibu wa SHIVYAWATA
Mkoa wa Dodoma, Bw. Justus Ng’wantalima alimpongeza Naibu Waziri kwa jitihada
ambazo amekuwa akizifanya katika kutetea Watu wenye Ulemavu.
Katika
ziara hiyo Naibu
Waziri Ikupa, alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya, Chama cha Walemavu Sulungai kinachojishughulisha na
ushonaji wa viatu vya wazi (kobasi) na utengenezaji wa majiko.
Vilevile Mhe. Ikupa alitembelea shule ya Viziwi iliyopo Jijini Dodoma.
Post a Comment