GEREZA LA KWITANGA LIPATIWE KIWANDA CHA KISASA-MAJALIWA

WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe
gereza la Kwitanga mkoani Kigoma linapata kiwanda bora na cha kisasa
cha kukamulia mafuta ya mawese kitakachoonesha dhamira ya Serikali ya
kufufua zao la michikichi nchini.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na
Jeshi la Magereza katika kuboresha shamba lake la michikichi pamoja na
mabadiliko waliyoyafanya kwenye kiwanda chao cha kuzalisha mafuta.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 17) wakati alipotembelea
Gereza la Kwitanga kwa ajili ya kukagua shamba la michikichi na kuzindua
trekta na kufungua sero moja iliyojengwa gerezani hapo.
Amesema
amefurahishwa baada ya kukuta mashine mpya ya kukamulia mafuta ya
mawese inafungwa kwenye kiwanda cha gereza hilo ambayo itakuwa inatumia
mota tofauti za zamani wapolikuwa wanatumia mashine ya kusukumwa na
mikono.
Kadhalika
Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO)
waimarishe teknolojia ya kukamua mafuta kwenye kiwanda hicho ili kiweze
kuzalisha kwa tija.
Katika
kuhakikisha gereza hilo linakuwa la mfano kwenye kilimo cha zao la
michikichi, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
inunue gari lenye winchi litakalorahisisha uvunaji wa chikichi.
Waziri
Mkuu amesema njia inayotumiwa kwa sasa ya kupanda juu ya mchikichi
wakati wa mavuno si salama kwa mvunaji, hivyo ni vema wakatumia magari
hayo yenye winchi kwa ajili ya kurahisisha shughuli ya uvunaji.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Leonard Burushi amesema wamefanikiwa
kuongeza uzalishaji wa mafuta kutoka pipa 63.4 kwa mwaka 2016/2017 na
kufikia pipa 97 kwa mwaka 2018/2019 na zoezi la uvunaji bado
linaendelea.
Amesema
mafanikio hayo yametokana na maagizo yalitolewa na Waziri Mkuu
alipotembelea gereza hilo Julai, 2018, ambapo pamoja na mambo mengine
aliwaagiza waboreshe eneo la kukamulia mafuta ili waongeze uzalishaji.
Kiongozi
huyo wa Magereza mkoa wa Kigoma amesema eneo la ekari 20 limetengwa kwa
ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kukamua mafuta ya mawese,
maghala ya kutunzia mafuta machafu na upanuzi wa kiwanda baadae.
Amesema
maelekezo mengine yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na Magereza ya
Kwitanga na Ilagala yaongeze eneo la mashamba yake kwa ajili ya kupanda
michikichi mipya ambalo limetekelezwa.
Amesema
tayari gereza la Ilagala limeandaa jumla ya ekari 150 zenye uwezo wa
kupandwa michikichi aina ya tanera 8,550 na Kwitanga ekari 400 ambazo
zitapandwa miche 22,800 ya michikichi aina ya tanera.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, FEBRUARI 17, 2019.
Post a Comment