DKT. MWANJELWA AMUONYA MWEKA HAZINA WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KOROGWE KWA UTENDAJI USIORIDHISHA
Mwambawahabari
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kali kwa Mweka Hazina wa Halmashauri
ya Wilaya ya Korogwe, Bw. Issai Mbilu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Fedha
na Biashara wa Halmashauri hiyo kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo
na kumtaka kuacha kiburi na kujirekebisha mara moja ili atekeleze majukumu
yake kwa kutenda haki.
Onyo hilo amelitoa wilayani Korogwe wakati wa kikao kazi na watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe
chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kukagua miradi ya TASAF na kujiridhisha
na utekelezaji wake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mweka Hazina huyo, kutokuwa kikwazo kwenye
malipo halali ya watumishi wenzie pamoja na kutoa sababu zenye mashiko
za kukataa kuidhinisha malipo ya watumishi kwa maandishi pindi anapobaini
mapungufu.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemsisitiza Mweka Hazina huyo kuacha kuipendelea
idara yake katika kulipa stahili mbalimbali ikiwamo posho ya saa za
ziada kazini na kuongeza kuwa malipo ya posho hiyo sio kwa ajili ya
watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee bali ni kwa ajili ya watumishi
wote wa halmashauri kwani ni haki kwa mtumishi yeyote aliyefanya kazi
katika muda wa ziada kulipwa stahili yake.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kwamba, kitendo cha kuwalipa posho
ya saa za ziada watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee kinashusha
morali ya utendaji kazi kwa watumishi wengine.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa halmashauri hizo
kutofanya udanganyifu ili wapate malipo yasiyostahili kwani ni kosa
kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma na kusisitiza
kuwa kila mtumishi afanye kazi kwa bidii ili alipwe anachostahili.
Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kwa mtumishi huyo ili ajirekebishe, ikiwa ni pamoja na kutoa somo kwa watumishi wote wa umma nchini
wanaofanya kazi bila kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Tanga yenye
lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi kwa umma, ikiwa ni
pamoja na kukagua na kujiridhisha na utekelezaji wa miradi ya TASAF
mkoani humo.
Post a Comment