Korosho Yaingiza Serikali fedha za Kigeni Zaidi ya Tsh. Trilioni Moja.
Zao la Korosho katika kipindi kilichoishia Januari
2018 liliingizia Taifa fedha za kigeni shilingi 1,136,609,586,722
ikilinganishwa na mazo mengine ya biashara.
Akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe.
Maftaha Abdallah Nachuma, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omari Mgumba, amesema
licha mchango huo katika uchumi wa Taifa, zao la korosho limekuwa likikabiliwa
na changamoto mbalimbali ambazo Serikali imekuwa ikizitafutia ufumbuzi ikiwemo
kuongeza bei ya korosho na kutafuta masoko ya uhakika.
Mhe. Mgumba amezitaja changamoto hizo kuwa ni
kuyumba kwa bei ya korosho katika soko la dunia kutokana na zao hilo kuuzwa
likiwa ghafi yaani bila kuongezwa thamani, tija ndogo katika uzalishaji, baadhi
ya wakulima kutotumia miche bora na matumizi hafifu ya pembejeo ikiwemo
viuadudu kama salfa na wakulima kutozingatia kanuni bora za kilimo katika
uzalishaji.
Aidha, Mhe. Mgumba amezitaja changamoto nyingine
kuwa uvunaji na uhifadhi hafifu wa korosho, uwezo mdogo wa maghala ya
kuhifadhia korosho na baadhi ya wakulima kuchanganya zao hilo na mawe na
mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito wakati wa mavuno.
“Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali
imeboresha mfumo wa uuzaji wa korosho kwa kuimarisha usimamaizi na ukaguzi
kuanzia ngazi ya vyama vya msingi, maghala makuu, maghala aya hifadhi na kutoa
elimu, kurejesha kwa kiwanda cha BUCCO cha mkoani Lindi cha ubanguaji wa
korosho, ujenzi wa maghala matatu ya kuhifadhia korosho katika mikoa ya Lindi,
Pwani na Tanga ili kuongeza kiwango cha uhifadhi na ubora wa korosho pamoja na kuzalisha miche bora
10,000,000 na kuisambaza kwa wakulima bure,”alisema Mgumba.
Naibu Waziri Mgumba ameongeza kuwa mikakati
mingine ni pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika zao la korosho ili
kuongeza uzalishaji, kuimarisha usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati,
kutoa huduma za ugani pamoja na kuweka mazingira wezeshi na kuwajengea uwezo
wabanguaji wa ndani kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho inayozalishwa
nchini.
Akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa
Mtama, Mhe. Nape Nnauye aliyetaka kujua hatua zilichukuliwa na Serikali kuhusu
vitendo vya rushwa katika kuhakiki ununuzi wa Korosho, Waziri wa Kilimo, Mhe.
Japhet Hasunga alisema kuwa wote
waliojihusisha na vitendo hivyo hatua kali zilichukuliwa dhidi yao ikiwemo
kusimamishwa kazi.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa na dhamira ya
dhati ya kuwainua wakulima nchini ikiwemo wa korosho kwa kuongeza bei ya
korosho na kusimamia ununuzi wake. Jambo ambalo limekuwa kichocheo kwa wakulima
wengi katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Tanga kujikita katika kilimo
hicho.
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwishoni mwaka
2018 alisema Serikali itanunua korosho kwa bei ya shilingi 3,300 kwa kilo.
Jambo ambalo lilifanyiwa kazi na wakulima wa zao hilo wanafurahia bei hiyo na
kutambua kuwa Serikali inawajali.
Post a Comment