Rais Magufuli Apokea Hati Za Utambulisho Kutoka Kwa Mabalozi Wa Misri Na Ethiopia
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe
10 Desemba, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 2 kutoka nchi
za Ethiopia na Misri walioteuliwa kuziwakilisha nchi hizo hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Yonas Yosef Sanbe – Balozi wa Ethiopia hapa nchini na Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa – Balozi wa Misri hapa nchini.
Mabalozi
hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwakaribisha hapa nchini na
wameahidi kuwa katika kipindi cha uwakilishi wao watahakikisha
wanaimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa nchi hizo na
Tanzania hususani kusimamia kwa ukaribu ushirikiano katika maeneo ya
kiuchumi.
Mhe.
Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kufikisha salamu zake kwa viongozi
wakuu wa nchi hizo na kubainisha kuwa Tanzania ipo tayari kwa
ushirikiano zaidi utakaoleta manufaa kwa wananchi wa nchi zote.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa wa Canada Mhe. Marc-Andre
Fredette, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada
ya mazungumzo hayo Mhe. Fredette ambaye anashughulikia Wizara 3 za
Canada (Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Biashara za Kimataifa na
Wizara ya Maendeleo) amepongeza maendeleo makubwa ambayo Tanzania
imeyapata na amesema Tanzania na Canada zinaendelea kushirikiana katika
maeneo mbalimbali yakiwemo katika sekta ya afya na elimu kwa ufanisi
mkubwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
10 Desemba, 2018
Post a Comment