SERIKALI IMEANDAA MPANGO WA KUPUNGUZA UKATILI –MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeandaa Mpango
wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto kwa lengo la
kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii kwa
asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo
ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005);
Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA
(1998).
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Novemba 25, 2018) wakati akizindua
Kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsiakatika Uwanja vya Jamhuri
jijini Dodoma. Amesema katika kukabialia na ukatili wa kijinsia Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imekuwa ikichukua hatua
mbalimbaliza kuzuia na kutokomeza ukatili.
Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mpango huo utachangia katika
utekelezaji wa mipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa
kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.
Kadhalika Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Mikoa
wote wahakikishe wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na
Watoto za ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji kama inavyoelekezwa
katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya
Wanawake na Watoto.
“Vilevile, nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
kuanzisha Programu za Kijamii za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika
Halmashauri husika zitakazozingatia hali halisi na kuzitengea bajeti programu
hizo kama inavyoelekezwa kwenye Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili
Dhidi ya Wanawake na Watoto. “
Pia Waziri Mkuu amesema watu wenye ulemavu wana mahitaji
maalumu na ni wahanga wa ukatili wa kijinsia ameelekeza Jeshi la Polisi
kuboresha Dawati lake la jinsia ili liweze kushughulikia kikamilifu masuala ya
ukatili wa kijinsia dhidi ya watu wenye ulemavu. “Hivyo, kuanzia sasa Dawati
hilo liitwe Dawati la Polisi la Jinsia, Watoto na Watu wenye Ulemavu.”
Akizungumzia kuhusu maana ya ukatili wa kijinsia amesema ni hali
ya kutenda vitendo viovu, vinavyodhalilisha, vinavyotesa, vinavyonyanyasa,
vinavyokandamiza, visivyojali haki za kuishi kwa binadamu anaweza kuwa wa kiume
au kike.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema ukatili wa kijinsia huja katika
taswira nyingi. “Aidha, kwa uchache tunapozungumzia ukatili wa kijinsia
tunamaanisha vitendo kama vile, vipigo, ubakaji, ukeketaji, ulawiti, matusi,
lugha na vitendo vya udhalilishaji pamoja na kunyimwa fursa za kushiriki katika
shughuli za kiuchumi.”
“Hivyo, ukatili wa kijinsia ni unyanyasaji wowote unaofanywa na
mtu dhidi ya mtu mwingine bila kujali umri, maumbile, kabila, rangi, dini au
mtazamo wa kisiasa. Unyanyasaji huu unahusisha mambo mengi kama kumpiga
mwanamke au mwanamme, kumnyima mtoto elimu, kumlawiti mtoto wa kike au kiume,
kumbagua mtu katika mahitaji ya msingi au kuwanyima urithi warithi
wanaohusika.”
Aidha, taarifa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuwahudumia Watoto (UNICEF) za mwaka 2017 zinaonesha kuwa wanawake na wasichana
wapatao milioni 750 Duniani waliolewa wakiwa chini ya miaka 18. Halikadhalika,
taarifa hiyo inakadiria kuwa wasichana milioni 120 (yaani mmoja kati ya
wasichana 10) Duniani wamekumbana na vitendo vya kulazimishwa kufanya ngono
bila ridhaa yao.
Waziri Mkuu amesema kama zilivyo nchi nyingine Duniani, Tanzania
ni miongoni mwa nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukatili wa kijinsia na
kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka
2015/2016 kupitia inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya
miaka 15 - 49 wamefanyiwa ukatili wa kupigwa au kingono katika kipindi cha
maisha yao.
(Mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPilI, NOVEMBA 25, 2018.
Post a Comment