Mbowe amtaka Rais Magufuli kuwawajibisha wahusika ajali ya MV Nyerere

Mwenyekiti
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amemtaka
Rais John Magufuli, kuwawajibisha waliohusika kwa namna moja ama
nyingine kusababisha ajali ya kuzama kwa Kivuko cha MV Nyerere,
iliyotokea jana Ukerewe mkoani Mwanza.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Septemba 21,
Mbowe amesema Rais Magufuli achukue hatua hiyo haraka kwani
amewawajibisha watu wengi kwa sababu mbalimbali kwenye hili pia afanye
hivyo.
“Na asiseme hachukui hatua kwa sababu amesema Mbowe, hili ni suala la kitaifa ndugu zetu wamefariki, ni msiba wetu.
“Huu
ni msiba wa kitaifa tunamtaka Rais Magufuli pia azungumze na taifa,
isitoshe tu Msigwa wa Ikulu (Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
Gerson Msigwa) kutoa taarifa TBC kwamba rais anatoa pole, azungumze na
Watanzania awape pole tunaamini atautambua ni msiba wa taifa na atangaze
maombolezo,” amesema Mbowe.
Aidha,
amesema serikali ijiandae fidia kwani utaratibu wa kawaida wa vyombo
vya usafiri vinakatiwa bima na kwamba kivuko kile lazima kimekatiwa
kwani ni kivuko kinachobeba roho za watu hivyo ni lazima watengenezewe
utaratibu wa bima ili wanapopoteza maisha familia zao lazima zilipwe
fidia lakini kwa sababu hakuna watu wanaowajibika utaratibu huo
haufanyiki.
“Sisi
kama chama tutashiriki kuomboleza katika msiba huu tunasubiri taarifa
kama kutakuwa na mazishi ya halaiki au misa maalumu, tunasubiri kwa
unyenyekevu tuungane kuwasindikiza wenzetu hawa ambao wametangulizwa
mbele ya haki kwa uzembe wa watu wachache,” amesema.
Post a Comment