WANAMISUNGWI TUMIENI VIZURI FEDHA ZA PAMBA-DC .
MKUU wa wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Bw.
Juma Sweda amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatumia
vizuri fedha wanazozipata kutokana na mauzo ya zao la pamba.
Amesema
ni vema wakatumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo katika
familia zao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba bora na za kisasa na
wawaendelea watoto kielimu.
Mkuu
huyo wa wilaya ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 11, 2018) wakati
akiwa kwenye ziara ya kukagua shughuli za uvunaji na uuzaji wa zao la
pamba. Ziara hiyo imefanyika kwenye vijiji vitatu vya kata ya Mondo
wilayani hapa.
Bw.
Sweda amesema wananchi wengi walihamasika kulima zao la pamba baada ya
Serikali kuhamasisha walime na kuahidi kulifuatilia kuanzia hatua za
utayarishaji wa mashamba hadi utafutaji wa masoko.
“Naishukuru
Serikali kwani baada ya kuhamasisha ufufuaji wa kilimo cha zao la pamba
nasi tuliungana na wananchi kuhakikisha maelekezo hayo tunayatekeleza
kwa vitendo, lengo letu kubwa ni kuona zao hilo linarudi kama zamani,”
amesema.
Amesema
kwa sasa wapo katika hatua ya uvunaji na uuzaji, ambapo wamejipanga
kukagua kikamilifu ili kuona zoezi hilo linaenda vizuri na pamba yote
inayopokelewa na vyama vya Ushirika ni ile iliyo katika ubora
unaohitajika.
Amesema
viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) hukagua pamba kabla
ya kuipokea na iwapo mkulima atabainika kupeleka pamba chafu hulazimika
kuisafisha kwanza kwa kutenga safi na chafu ndipo hupima na kulipwa.
Mkuu
huyo wa Wilaya ameongeza kuwa, mbali na kukagua usafi, pia wanasimamia
zoezi la malipo kwa wakulima na kuhakikisha kwamba wanaouza pamba wote
wanalipwa hapo hapo na ni marufuku mnunuzi kumkopa mkulima.
Kwa upande wake,
Afisa Kilimo wa Kata ya Mondo, Bw. Sebastian Mbandi amesema mafanikio
ya zao hilo kwa mwaka huu ni makubwa ukilinganisha na miaka iliyipita,
hata hivyo wameshindwa kufikia malengo waliyojiwekea kutokana na mazao
mengi kushambuliwa na wadudu aina ya thrips.
Bw.
Mbandi amesema walitarajia kuvuna wastani wa tani 1.5 kwa ekari moja
lakini kutokana na changamoto ya ugonjwa iliyosababishwa na mdudu huyo
wanatarajia kuvuna wastani wa kilo 800 kwa ekari.
Kwa upande wao,
wakulima ambao walizungumza kwa nyakati tofauti, walitumia fursa hiyo
kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa kuhamasisha wananchi walime zao
la pamba, ambapo nao waliitikia wito huo na sasa wameanza kuona
mafanikio.
Miongoni
mwa wakulima hao ni pamoja na Bw. Hoja Ngole mkazi wa Kijiji cha Mondo
ambaye amelima ekari sita na tayari ameshavuna na leo ameenda kuuza na
anatarajia kutumia fedha atakazozipata kwa kujenga nyumba ya kisasa.
Bw.
Ngole na mkewe Bibi Sara wameahidi kuongeza ukubwa wa shamba katika
msimu ujao na wamewaomba wananchi wengine kuchangamkia fursa ya kulima
zao hilo kwa kuwa ni mkombozi wa maisha yao.
Naye,mkulima
mwingine Bw. Michael Masalamunda ambaye alikuwa amepeleka pamba yake
katika kituo cha mauzo cha Mwanimo AMCOS amesema anatarajia kutumia
fedha atakazozipata baada ya mauzo hayo kwa kuongeza mtaji wa biashara
ya ng’ombe.
Bw.
Masalamunda naye amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kuwahamasisha
walime zao la pamba pamona na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye
aliwahamasisha na kufuatilia maendeleo ya zao hilo.
Pia
ameishukuru Serikali kwa kuagiza mauzo ya zao hilo yasimamiwe na vyama
vya Ushirika kwa sababu vimewezesha wakulima kuwa na soko la uhakika la
pamba yao na wakiuza tu wanalipwa fedha zao hakuna anayekopwa. “Mimi leo nakuja kuuza kwa awamu ya pili na fedha zote nimelipwa,”.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, Juni 11, 2018.
Mkulima wa pamba katika kijiji cha Mondo
wilayani Misungwi, Hoja Ngole akitumia mkokoteni wa kokotwa na ng’ombe
kupeleka pamba yake kuuza kwenye Chama cha Ushirika wa Mwaniko katika
kijiji cha Mondo Juni 11, 2018. Uuzaji wa pamba wilayani Misungwi
unaendelea vizuri na kilo moja inauzwa kwa sh. 1100/=. (Picha na ofisi
ya Waziri Mkuu)
Post a Comment