WAGONJWA 15 KATI YA 20 WAFANYIWA UPASUAJI WA MOYO KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU YA MOYO INAYOENDELEA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bashir Nyangasa akiwaonyesha waandishi wa habari jinsi upasuaji wa kurekebisa mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair) unavyofanyika katika kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya Mjini Mumbai nchini India. Hadi sasa jumla ya wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
...................................................................................
Jumla ya wagonjwa 15 wamefanyiwa upasuaji
wa moyo wa kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu ya moyo ya siku
sita inayofanywa na madaktari bingwa wa
upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya
mjini Mumbai nchini India .
Wagonjwa hao wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG
– Coronary Artery Bypass Grafting), kubadili milango miwili hadi mitatu ya moyo (Valve Replacement) na upasuaji wa
kurekebisha mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili
(Aortic Aneurysm Repair/Bental Procedure).
Aidha katika kambi hii kwa mara ya kwanza umefanyika
upasuaji wa kuvuna mshipa wa damu ndani
ya kifua upande wa kulia na kushoto na kuunganisha kwenye misuli ya moyo ili
kuuongezea moyo damu.
Wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji hali
zao zinaendelea vizuri na saba kati yao wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na
kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu.
Katika kambi hiyo iliyoanza tarehe 18 na
inatarajiwa kumalizika tarehe 23 mwezi
huu inaenda sambamba na utoaji wa elimu
pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa madaktari wetu pamoja na wauguzi. Jumla
ya wagonjwa 20 ambao ni watu wazima
wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.
Tunawaomba wananchi waendeleee kuchangia damu
kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu kati ya
chupa sita hadi saba wakati
wanapatiwa matibabu. Taasisi inamkaribisha
mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu
ambao wanapenda kuchangia damu waweze kufanya hivyo ili tuokoe maisha ya ndugu
zetu wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
21/06/2018
Post a Comment