WAFANYABIASHARA 500 TANZANIA NA MALAWI WAKUTANA JULAI 26 MWAKA HUU MKOANI MBEYA.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
MWAMBA WA HABARI
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Wafanyabiasha nchini wametakiwa kushiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi linalotarajiwa kufanyika Julai 26 hadi 27 mwaka huu Mkoani Mbeya.
Kongamano hilo limeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan,Trade), Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Malawi (MITC), huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla, amesema kuwa kongamano hilo linatarajia kuwakutanisha wafanyabishara/wawekezaji 500 kutoka Taasisi za umma na sekta binafsi kutoka Tanzania na Malawi.
Amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja wafanyabiashara/wawekezaji wa nchi mbili ili kubuni fursa mbalimbali za kibiashara na uwekezaji zitakazowezesha kuanzisha na kuendelea miradi katika sekta za mbalimbali ikiwemo viwanda, usafirishaji, utalii pamoja na elimu.
"Kupitia kongamano hilo tutafanikiwa kuendeleza sekta ya uvuvi, kilimo , madini, afya, benki, mawasiliano na tehama" amesema Mhe. Makalla.
Mhe. Makalla amefafanua kuwa wafanyabiashara watapata fursa mbalimbali za kibiashara ikiwemo kufanyika mikutano kati ya serikali na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Malawi.
"Katika kongamano hilo kauli mbiu ni Kuimarisha Uhusiano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Malawi" amesema Mhe. Makalla.
Ameeleza kuwa kongamano hilo linafanyika Mkoa wa Mbeya kutokana mkoa huo kwa sasa kuna mazingira rafiki ikiwemo miundombinu pamoja na kuunganisha mikoa mengine na nchi Jirani ikiwemo Malawi na Zambia.
Katika hatua nyengine amebainisha kuwa serikali kupitia mkoa wa Mbeya tayari wamefungua milango ya uwekezaji kwa kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi ikiwemo meli mbili za kisasa za mizigo na abiria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Godfrey Simbeye amesema kuwa nchini Malawi kuna fursa nyingi za uwekezaji, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wa Tanzania tayari wameanza kuwekeza nchini humo.
Godfrey ameeleza kutokana na fursa zilizopo wafanyabiashara wanapaswa kujitokeza katika kushiriki kongamano hilo ambalo litawakutanisha wafanyabiashara wa nchi mbili.
"Wafanyabiashara wanapaswa kujitokeza..pia tunaomba serikali kuendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji ili tuendelee kupiga hatua" amesema Godfrey.
Kongamano hilo linawapa fursa wafanyabishara wote kushiriki bure, hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kujaza fomu ya usajili kupitia tovuti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambayo ni www.Mbeya.go.tz na baadaye kuziwasilisha kwa barua pepe kupitia; ras.mbeya@mbeya.go.tz.
Aidha kupitia TIC htt: www.tic.go.tz/ displayPublication na baadaye kutuma kwa; diana.ladislaus@tic.go.tz.
Post a Comment