TRA YATAIFISHA BOKSI 41 ZA MVINYO NA POMBE KALI DODOMA
Mwamba wa habari
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere akiangalia chupa ya pombe kali aina ya Jameson katika duka la jumla Jijini Dodoma kuangalia kama chupa hiyo ina Stepu ya Kodi wakati akifanya ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye maduka na vituo mbalimbali vya mafuta.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere akifungua boksi katika duka la jumla Jijini Dodoma kuangalia
kama vinywaji vilivyomo kwenye boksi hilo vina Stepu za Kodi wakati akifanya
ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye
maduka na vituo mbalimbali vya mafuta.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere akizungumza na Dereva wa Bodaboda Issa Athumani ambaye
amekamatwa na Kamishna huyo na kumtoza faini ya shilingi 30,000 kwa kosa la
kununua mafuta bila kudai wala kuchukua risiti Jijini Dodoma wakati akifanya
ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye
maduka na vituo mbalimbali vya mafuta.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.
Charles Kichere akiangalia risiti ya kielektroniki ya EFD wakati akifanya
ukaguzi wa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwenye
maduka na vituo mbalimbali vya mafuta Jijini Dodoma. Mwenye Kanzu nyeupe ni
Msimamizi wa Kituo cha Mafuta cha Camel Oil kilichopo maeneno ya Kisasa. (PICHA
NA TRA).
Na
Veronica Kazimoto - Dodoma
Mwamba wa habari
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imekamata na kutaifisha boksi 41 za mvinyo na pombe kali zilizokutwa
katika duka la jumla jijini Dodoma zikiwa hazina Stempu za Kodi.
Boksi hizo zenye thamani ya
shilingi milioni tatu ambazo ni mali ya Anthony George, zimekamatwa na
kutaifishwa leo wakati Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere akikagua matumizi
ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) Jijini hapa kwenye maduka
na vituo mbalimbali vya mafuta.
Akizungumza mara baada ya
kutaifisha boksi hizo, Kichere amesema kuwa, ni wajibu wa muuzaji kuhakikisha
kwamba, vinjwaji vinavyostahili kuwekewa Stempu za Kodi vinakuwa na stempu hizo
ili kuisaidia Mamlaka kutoza kodi stahiki.
"Inatakiwa Stempu za Kodi
ziwekwe kwenye mzigo kabla mzigo huo haujanunuliwa na wauzaji wa rejareja. Hii
itaisaidia TRA kukusanya kodi halali na hatimaye kuongeza ukusanyaji wa mapato
ya Serikali," alisema Kichere.
Mvinyo na pombe kali zilizokamatwa
na kutaifishwa ni pamoja na boksi 27 za Robertson, boksi 7 za Jameson, boksi 5
za Drostdy Hof na boksi 2 za Alko Dompo.
Wakati huo huo, Kamishna
Mkuu Kichere amemkamata Dereva wa Bodaboda Issa Athumani na kumtoza faini ya
shilingi 30,000 baada ya kununua mafuta ya bodaboda hiyo bila kudai wala
kuchukua Risiti ya Kielektroniki ya EFD.
Kichere ameeleza kuwa, wananchi
ambao hawadai risiti wanatakiwa kutozwa faini ya shilingi 30,000 hadi 1,500,00
au kuhukumiwa kifungo kisichozidi miezi
sita kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015.
"Kuna watu ambao
hawadai risiti na kuna mwingine nimemkamata leo ambaye nimemtoza faini ya
shilingi 30,000 ili iwe fundisho kwa watu wote wanaonunua bidhaa na huduma
mbalimbali bila kudai wala kuchukua risiti", aliongeza Kichere.
Aidha, Kamishna Mkuu Kichere
ametoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kutoa risiti kila wanapofanya mauzo
na wananchi kuhakikisha wanadai risiti kila wanapofanya manunuzi mbalimbali.
"Natoa wito kwa wafanyabiashara
wote waendelee kutoa risti lakini pia wanunuaji wadai na kuchukua risiti.
Tunataka kujenga utamaduni wa kutoa na kudai risiti ili tuweze kukusanya kodi
stahiki," alisema Kichere.
Naye, Mfanyabiashara wa
mafuta jijini hapa Faustine Mwakalinga amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa
kutembelea kituo chake cha mafuta na kusema kuwa, zoezi hilo analolifanya
litaongeza mapato ya Serikali kwasababu linajenga ukaribu na kutatua changamoto
zinazowakabili wafanyabiashara hao.
"Namshukuru sana
Kamishna Mkuu wa TRA kwa kutembelea
kituo changu cha mafuta na nimefurahishwa sana na jinsi anavyofanya kazi yake ukizingatia
leo ni sikukuu. Ukaguzi huu anaoufanya
Kamishna Mkuu, utasaidia kuongeza mapato ya Serikali na kusaidia kutatua changamoto
mbalimbali zinazotukabili sisi wafanyabiashara," alifafanua Mwakalinga.
Kamishna Mkuu Kichere
ametembelea jumla ya Vituo vya Mafuta vinane na maduka 15 ikiwa ni moja ya
utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Mpango wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni
Dodoma hivi karibuni.
Post a Comment