MAMENEJA WA TRA NCHINI WAAGIZWA KUWATEMBELEA WAFANYABIASHARA MARA KWA MARA
Na Veronica Kazimoto
Dodoma
Mwamba wa habari
Mameneja wote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nchi nzima wameagizwa kuwa na utaratibu wa kuwatembelea wafanyabiashara mara kwa mara ili kujua changamoto zao na kuzitatua ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara hao.
Agizo hilo limetolewa leo na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere jijini Dodoma alipohitimisha ziara yake ya kikazi ya kujiridhisha utendaji kazi wa Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) ambazo mfumo wake ulipata hitilafu ya kiufundi hivi karibuni na kusababisha mashine hizo kutokufanya kazi.
"Nimepita katika baadhi ya maeneo mengi kuanzia Dar es Salaam, Kibaha, Mlandizi, Morogoro, Gairo na sasa nimemalizia Dodoma. Katika maeneo yote niliyopita nimekuta wafanyabiashara wana changamoto ambazo zinaweza kutatulika kirahisi na Mameneja bila ya kusubiri mpaka Kamishna Mkuu apite, hivyo nawaagiza Mameneja kuwatembelea wafanyabiashara katika maeneo yao, kujua changamoto wanazozipata ili kuzitatua mara moja kinyume na hapo nitachukua hatua," alisema Kichere.
Aidha, Kamishna Mkuu Kichere alieleza kuwa, tatizo la Mashine za EFD limekwisha na tayari zimeanza kufanya kazi, hivyo Mameneja wote wa mikoa wanatakiwa kupita katika maeneo yao ili kufanya ufuatiliaji wa mashine hizo na kuzitolea taarifa zile zitakazokutwa bado zina matatizo kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
"Ninasema Mameneja wawatembelee wafanyabiashara mara kwa mara kwasababu nimepita katika maduka mbalimbali nimekuta kuna baadhi ya wafanyabiashara tangu Mfumo wa EFD upate hitilafu mpaka leo hawajawasha mashine zao na nilipoziwasha nimekuta zinafanya kazi vizuri, hivyo kinachotakiwa ni Mameneja kupita katika maeneo yao na kufanya ukaguzi wa mashine husika na kuwapa elimu," alifafanua Kichere.
Kamishna Mkuu Charles Kichere amehitimisha ziara yake iliyoanzia Dar es Salaam mpaka Dodoma akipita katika maduka na vituo mbalimbali vya mafuta kwa ajili ya kujiridhisha kama mashine za EFD zinafanya kazi vizuri baada ya mfumo wake kupata hitilafu ya kiufundi tangu Mei 11, mwaka huu kutengemaa na kuruhusu mashine hizo kuanza kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Post a Comment