Basi la Mahakama inayotembea kuwasili Agosti Dar
Mwambawahabari , Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa, Ibrahim Juma amesema ifikapo Agosti mwaka huu Basi la Mahakama inayotembea linatarajia kuwasili lengo likiwa kuwasogezea wananchi huduma za kimahakama kwa urahisi huku akibainisha kuwa mahakama inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchahce wa mahakimu na mazingira mabovu ya kufanyia kazi.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es Salaam wakati Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia(WB), Sandie Okoro alipotembelea mahakama kwa ajili ya kuangalia utekekelezaji wa Mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na benki hiyo.
Amesema kutokana na mahakama kukumbwa na changamoto nyingi wameonelea kutumia njia mbadala za kupunguza msongamano wa watu wanaohitaji msaada wa kisheria hasahasa zinazotumiwa na nchi zilizoendelea ikiwemo mabasi ya mahakama inayotembea na meli.
“Kuna watu wameshaenda Afrika Kusini kuangalia muundo wa basi litakavyokuwa tunaamini likiwasili litapunguza changamoto za kimahakama litakuja moja kwanza mkoani Dar es Salaam” amesema.
Amebainisha kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo wataanza na basi hilo na kwamba baadaye wataangalia utaratibu wa kuongeza mengine katika mikoa mingine.
Amesisitiza kuwa katika Mkutano utawaokutanisha Majaji, Wanasheria na Mahakimu mkoani Arusha kuanzia Juni 11 hadi 13 mada kubwa itakayojadiliwa itaangalia ni kwa jinsi gani haki inatendeka bila kuangalia jinsia.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Okoro amefurahishwa utendaji kazi wa mahakama nchini na kuitaka kuongeza juhudi za dhati kutatua matatizo yanayoikabili.
Katika hatua nyingine makamu huyo baada ya mazungumzo ya ukaribisho mchana ametembelea Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni kujionea jengo na shughuli za mahakama hiyo zinavyoendeshwa.
Post a Comment