UCHAGUZI KINONDONI HAPATOSHI, CHADEMA YAONYA VIAPO VYA MAWAKALA.
Mwambawahabari
Chama cha Chadema kimemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, RPC Jumanne Mlilo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kumchukulia hatua Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni (OCD) anayedaiwa kuamuru unyanyasaji wa wanachama wa chama hicho.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mafunzo na Operesheni Chadema, Benson Kigaila amedai kuwa jana polisi waliwapiga na kuwkamata baadhi ya vijana wao bila ya makosa, ambapo pia diwani wake aliyemtaja kwa jina la Mgawe alipigwa kichwani na kitako cha bunduki na kuzimia.
“Jana saa moja jioni Polisi walituvamia hapa ngome ya chama chetu na kupiga mabomu,kujeruhi wanachama na viongozi wetu,wakati haya yakifanyika tulikuwa ndani tumekaa kikao na wabunge wetu. Polisi wamekamata wanachama wetu jumla 19.Hatukuwa na tatizo lolote lile wala mvutano wowote ule baada ya kumaliza mikutano yetu miwili,” amesema.
Akifafanua kiini cha tuki hilo, Kigaila amedai baadhi ya wafuasi wa Chadema waliwakuta watu wanaodaiwa kuwa wa CCM wakikusanya shahada za wapiga kura na kuzitoa kopi kwa ajili ya kuwatengenezea watu ambao si wakazi wa Kinondoni ndipo walipowakamata watu hao.
Amedai kuwa, baada ya kuwakamata, watu hao waliwapigia simu polisi na kwamba baada ya polisi kufika wakaanza kuwashambulia vijana wa Chadema na kukamata baadhi yao.
“Wakati polisi wanawapiga vijana wetu ccm walimmwagia spray vijana wetu machoni na kuwasababishia maumivu makubwa,Diwani wetu Mgawe amepigwa kichwani na kitako cha bunduki mpaka akazimia hadi akapelekwa hospitali,huu unyama wa polisi dhidi yetu unapaswa kuchukuliwa hatua,tunamtaka RPC wa Kinondoni,na IGP wamchukulie hatua huyu OCD aliyeamuru huu unyanyasaji,” amesema.
Kufuatia madai hayo, mtandao Darmpya.com ulimtafuta RPC Jumanne kwa njia ya simu kwa ajili ya ufafanuzi wa matukio hayo, ambapo amesema taarifa hizo ni za uongo, na kwamba polisi hawakuvamia ngome yao, na vijana waliokamatwa ni 15 ambao walikuwa wanafanya fujo barabarani baada ya kampeni kuisha.
Post a Comment