TRA YATAIFISHA TENA GARI NA BIDHAA MPAKANI NAMANGA
Arusha
Mwambawahabari
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mara nyingine ndani ya wiki mbili imekamata na kutaifisha tani moja ya sukari, mafuta ya kupikia katoni 10 na gari lililotumika kusafirisha bidhaa hizo kutoka nchini Kenya kupitia njia za magendo mpakani Namanga mkoa wa Arusha.
Meneja Msaidizi wa Forodha mkoani hapo Edwin Iwato alisema bidhaa hizo zimekamatwa usiku wa kuamkia leo na ni mali ya mfanyabiashara Paul Swai, ambaye alitumia gari namba T 496 AFE Nissan Carravan mali ya Christian Nko ambalo limetaifishwa pamoja na bidhaa husika.
"Tumemkamata mfanyabiashara mwingine aitwae Paul Swai akiwa anaingiza nchini bidhaa kutoka Kenya kuelekea mkoani Arusha kupitia njia za magendo bila kibali wala kulipa ushuru wa Serikali", alisema Iwato.
Iwato amefafanua kuwa tani moja iliyokamatwa ambayo ni mifuko 20 ya sukari ina thamani ya shilingi 2,200,000 na mafuta ya kupikia ambayo ni kilogramu 12 yana thamani ya shilingi 520,000.
Mfanyabiashara huyo pamoja na dereva wa gari lililotaifishwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ya Forodha na bidhaa hizo baada ya kukaguliwa na kugundulika kuwa zinafaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa kwa taasisi mbalimbali za Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu zilizowekwa na TRA.
Hii ni mara pili katika mwezi huu ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania imekamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali zikitokea nchini Kenya kupitia njia za magendo mpakani Namanga mkoa wa Arusha.
Post a Comment