Ads

Polisi 105 waadhibiwa kwa kupiga Raia

Jeshi la Polisi limewachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu askari wake 105 ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi.

Akizungumza bungeni leo Februari 9, 2018 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema askari hao wamechukuliwa hatua katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2017.

Masauni ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda aliyehoji iwapo kuna sheria yoyote ya nchi inayomruhusu polisi  kumkamata mtuhumiwa na kabla ya kumfikisha kituoni kumpiga na kumtesa bila kujua kosa lake.

"Je Serikali inachukua hatua gani za kuhakikisha askari wanaofanya vitendo kama hivyo wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi na mpaka sasa askari wangapi wamechukuliwa hatua za kisheria kutokana na makosa ya kujichukulia sheria mkononi," amehoji Mwakagenda.

Katika majibu yake, Masauni amesema kwa mujibu wa mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kifungu cha 11 kinaelekeza namna ya ukamataji, kwamba kifungu hicho hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia wakati wowote anapokuwa kizuizini.

Masauni amesema kanuni za utendaji wa jeshi la polisi (PGO) askari yoyote anapobainisha kufanya vitendo vya kupiga au kutesa raia huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa kazi au kufikishwa mahakamani.

No comments