Ads

MEYA ILALA AFUTA USHURU NA KODI KINYUME CHA SHERIA MASOKO YOTE MANISPAA YA ILALA.

Mwambawahabari
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala  Charles Kuyeko amepiga marufuku utozaji wa kodi, ushuru na tozo ambazo hazipo kisheria. Marufuki hiyo ameitoa leo  katika Soko la Ilala boma.

Sambamba na hilo,amefuta zoezi la upangishwaji wa vizimba kwa wafanya biashara wa Soko hilo kwani ni kiashiria cha kunyanyasa wafanyabiashara na marufuku hii naitoa si tu kwa soko la Ilala bali ni kwa masoko yote yaliyo chini ya Manispaa ya Ilala.

Masoko yote yaliyo chini ya mamlaka ya Manispaa inayoongozwa na mimi (Kuyeko) kuanzia leo ni marufuku kutoza wafanyabiashara kodi, ushuru na tozo kinyume cha sheria na masharti ya mikataba ya zabuni yafuatwe na kama kuna mikataba yenye kubeba maslahi ya mtu binafsi tutaifuta bila kusita, alisema Kuyeko.

Hayo ameyasema leo Jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kutembelea Soko la Ilala.


Katika ziara hiyo ambayo pia aliongozana na Naibu Meya wa Manispaa hiyo Omary Kumbilamoto, Mkurugenzi Msongela Palela, Katibu tawala (W) ya Ilala pamoja na wakuu wa idara huku wakipokelewa na Diwani wa Kata ya  Ilala ndugu Saady Khimji.

Meya Kuyeko pamoja na Mkurugenzi walifanya ziara hiyo kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya wafanya biashara wa Soko hilo juu ya uongozi wa soko hilo na mkandarasi.

Mara baada ya Meya na Msafara wake kuwasili,wafanya biashara walipata fursa ya kutoa dukuduku za kero na changamoto zinazowakabili mbele ya viongozi hao.

Akizungumza kwa niaba ya wafanya biashara wa mbogamboga sokoni hapo Mary Ramadhani amesema kuwa kero kubwa iliyopo sokoni hapo ni uongozi mbovu wa Soko ndio unaopelekea matatizo na kuibuka kwa makundi yasiyo rasmi.

Mary aliendelea kwa kusema, uongozi wa Soko kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wasio waaminifu kutoka Manispaa ya Ilala hususani Afisa masoko na Idara biashara, uongozi haukupatikana kihalali kwani viongozi waliopo walichaguli na watu 64 tu wakati soko lina watu zaidi ya 3000.

Uongozi badala ya kutetea haki na maslahi ya wafanyabiashara, chakushangaza viongozi ndiyo wanashirikiana namkandarasi kuandaa lisiti feki za malipo,utozaji wa tozo, ada na ushuru kinyume na sheria na matakwa ya mkataba wa zabuni, alisema Mary Ramadhan.

"Tunatozwa kodi mara tatu tunaponunua mzigo,getini na kwenye vizimba tunapouzia na kwa siku tunalipa takriban elfu saba kwa mtu mmoja kitu ambacho hakikubariki hivyo tunaomba ufafanuzi" na ofisi yako ichukue hatua, alisema Mary.

Naye Hamimu Juma mfanya biashara wa kuku amelalamikia uongozi huo kuwa, haufuati demokrasia na haukuchaguliwa na watu wote bali uliundwa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi.

Pia Hamimu amemweleza Meya kuwa, mkandarasi mwenye dhamana ya kusimamia soko hilo kuwa hafai kwani amekuwa akipandisha ushuru atakavyo,huku soko hilo likizidi kuteketea kwa uchafu hasa kipindi cha mvua.

Amesema,tangu uongozi huo ujikabidhi madaraka haujawahi kuitisha mikutano na wafanyabiashara, umekuwa ni uongozi wa kuamrisha bila kujari maslahi ya wafanya biashara ambao ndio walipa kodi.

Tunaomba mtusaidie kupata uongozi mpya kwani wafanya biashara tunateseka na faida yote inaishia kwenye Kodi huku Soko halina Maendeleo na kama mnavyoona miundombinu ni mibovu".

Mara baada ya wananchi hao kutoa kero zao juu ya uongozi ambao ndio chanzo cha matatizo yote,Naibu Meya Omary Kumbilamoto aliwatoa wasiwasi wafanya biashara hao kwa kuwaahidi kuyafanyia kazi waliyoyaeleza mara baada ya kupata maelezo.

Aidha, Mstahiki Meya Kuyeko akifunga kikao hicho alisema uongozi wake ni imara na tumejipanga kutatua kero zenu zote kwa haraka na ndiyo maana katika msafara wangu nimetembea na wataalamu wa idara akiwemo mkurugenzi, mwanasheria na afisa biashara na Mbele yenu namtaka mwanasheria akaiangalie sheria juu ya mkandarasi kwenda kinyume na masharti ya mkataba wa zabuni na wiki ijayo tunaweza kutoa majibu ya nini kinaendelea juu ya mkandarasi huyo.

Wakati huo huo amemtaka Afisa masoko na Afisa biashara kufika ofisini kwake siku ya jumatatu ili apate Maelezo kutoka kwao ni kwa nini wameshindwa kumsimamia mkandarasi wa soko la Ilala na ikibainika kunauze wa aina yeyote Baraza nlitachukua hatu kali dhidi yao.
Na Alex Massaba
Katibu ofisi ya Meya Manispaa ya Ilala
0656568256

No comments