MAPITIO YA TAARIFA NA MATUKIO MBALIMBALI YA WIKI YALIYORIPOTIWA KUHUSIANA NA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI)
Mwambawahabari
Hii ni wiki ya pili sasa kukuletea mukhtasari wa majumuisho ya mapitio ya taarifa na matukio na misimamo ya Chama juu ya masuala mbalimbali yaliyoripotiwa yanayohusiana na CUF kwa lengo la kuwajulisha wanachama, viongozi na watanzania kwa ujumla masuala yepi muhimu yanayoendelea ndani ya CUF na _-kuwekana sawa kwa kuwapa “updates” aidha kusahihisha taarifa za upotoshwaji/propaganda chafu dhidi ya Chama (CUF Weekly Reports).
KURUGENZI YA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA WIKI HII IMEPOKEA NA KUWALETEA TAARIFA ZIFUATAZO:
1. ZIARA YA KIKAZI YA KATIBU MKUU, MAALIM SEIF SHARI HAMAD KISIWANI PEMBA;
Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama Cha CUF ameendelea na ziara ya kikazi kisiwani Pemba iliyoanza tarehe 15/2/2017 na kupata mapokezi makubwa ya heshima na wanayoyaita ‘Mahaba Mubashara’ kutoka kwa wananchi wa kisiwa hicho. Maalim alikamilisha ziara kama hiyo kisiwani Unguja Tarehe 13/2/207.
Mpaka sasa ametembelea wilaya ya Chakechake na Mkoani na kufanya vikao na viongozi, wanachama wa wilaya na majimbo, amekutana na wabunge na wawakilishi na madiwani halali wa majimbo hayo waliochaguliwa na wananchi katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Viongozi wote hao wameonyesha wana hari na hamasa kubwa ya kuwatumikia wananchi wao na Chama chao na kamwe hawajarudishwa nyuma kwa vitendo vya hila vilivyofanywa na Mwenyekiti wa ZEC. Akiwa katika Jimbo la Ziwani alifungua tawi la Kichuwani, tawi ambalo limeanza na wanachama wapya mia tatu tisini (390) ikiwa ni ishara ya kukubalika na kuungwa mkono kwa CUF. Pia aliweka jiwe la msingi katika tawi la
Mgogoni jimbo la Wawi na ufunguzi wa tawi la Muharitani lililopo katika jimbo laChakechake.
Jana Tarehe 18/02/2017 aliendelea na ziara yake katika wilaya ya Mkoani, kwa kutembelea Jimbo la Chambani na Mtambile ambapo amekutana na watendeji wa chama na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Matawi mpaka wilaya. Mbunge wa Jimbo la Chambani ambae pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama- CUF Taifa Mhe. Yussuf Salim ametoa gari aina ya Toyota Townace kwa ajili ya kuboresha utendaji wa shughuli za chama. Pia Katibu Mkuu alifungua tawi la Mchakwe na Tawi la Chaleni katika jimbo la Kiwani.
Maalim amezinduzi na kuweka waratibu wa chama 694 katika wilaya ya ChakeChake, uzinduzi wa ofisi za Chama na kuweka mawe ya msingi katika majengo ya Chama katika maeneo mbali mbali ya kisiwa hicho. Katibu Mkuu amewahakikishia Wananchi wa kisiwa cha Pemba na watanzania kwa ujumla kuwa haki yao inayotokana na maamuzi halali waliyoyafanya katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 haitapotea na ipo karibu kupatikana. Katibu Mkuu amepokeza zawadi mbalimbali kutoka kwa wanachama na kuvishwa koja la ushujaa wa kuongoza mapambano ya kudai Haki kwa umahiri na weledi mkubwa na kwa njia za amani kinyume na matarajio washindani wetu ambao walijipanga kwa kufanya uharibifu, vurugu, umwagaji damu na hata mauaji kwa wananchi wasio na hatia.
Katibu Mkuu ameambatana katika ziara hiyo na Kaimu Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar Mhe Salim Bimani pamoja na viongozi wengine waandamizi wa kitaifa pamoja na Jumuiya za Chama JUKECUF, JUVICUF, na JUZECUF. Ziara hiyo itamalizika tarehe 24/2/2017 na baadae kuendelea kwa upande wa Tanzania Bara.
2. KUHUSU KESI ZA CHAMA ZINAZOENDELEA MAHAKAMANI NA MSIMAMO WA BODI YA WADHAMINI YA CUF:
(a) Kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamni ya Chama dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mtungi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lipumba na wenzake itaendelea Mahakama Kuu tarehe 21/2/2017.
Msimamo wa Chama katika kesi hiyo kumkataa Jaji Kihiyo kuendelea na kesi hiyo upo palepale mbali na yeye binafsi kung’ang’ania kuisikiliza kesi hiyo huku akiwa amekataliwa na amejidhihirisha wazi kuwa ana upande na maslahi binafsi yatakayokwaza misingi ya utendaji haki (for the interest of Justice) kama ataendelea kuisikiliza kesi hiyo. Bodi ya wadhamini ya CUF imewaagiza Mawakili wake kukatia Rufaa (Appeal) maamuzi (Ruling) ya Jaji Kihiyo aliyoitoa Tarehe 14/12/2016 na au kuomba kufanyia marejeo (Revision) maamuzi hayo.
Tarehe 19/12/2016 mawakili wetu waliiandikia Mahakama Kuu kuomba kupatiwa nyaraka za maamuzi hayo (Necessary Documents to start-up Appeal/Review process; Copy of Ruling, Proceedings and Drawn Order) kwa bahati mbaya tangu wakati huo mpaka sasa Jaji Kihiyo anaendelea na kufanyia ‘ Editing and Proof Reading’ ya documents hizo na mawakili wetu hawajapatiwa nakala ya nyaraka hizo.
(b) WANACHAMA WA CUF KUOMBWA KUTOHUDHURIA MAHAKAMANI TAREHE 21/2/2017:
Baaada ya mashauriano na mawakili wetu wametutaka tuwajulishe wanachama kuwa mnaweza kuendelea na shughuli zenu kwa kutohudhuria mahakamani siku ya kesi na muda huo mkautumia vyema katika majukumu mengine binafsi ya kila siku na ya ujenzi wa Chama.
Mawakili wetu watatuwakilisha ipasavyo na kwamba siku hiyo kutakuwa na kazi moja tu ya kuwasilisha dokomenti za kisheria na hakutakuwa na kinachoendelea kwa sababu muhusika Jaji Kihiyo ameshindwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati na tutamshangaa kama atamuua vinginevyo. Hata hivyo, mawakili wetu wamejipanga vyema kutuwakilisha na taarifa zote mtajulishwa kupitia vikao vya chama, vyombo vya habari na Mitandao ya kijamii. Msipoteze muda wenu kwa kwenda mahakamani kusikiliza kesi jinsi inavyoahirishwa, utakuwa ni uharibifu wa rasilimali fedha na muda.
(c) KUHUSU BODI YA WADHAMINI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-CHAMA CHA WANANCHI):
The Registered Trustees of The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) Bodi ya Wadhamini ya CUF ilisajiliwa rasmi kwa Kabidhi Wasii Mkuu wa Serikali Mwezi May, 1993 mara baada ya CHAMA kupata usajili wa kudumu kutoka kwa aliyekuwa Msajili wa vyama vya siasa nchini wa wakati huo Marehemu Jaji George Liundi (aliyekuwa na sifa ya kujiheshimu na kuheshimika na vyama vyote vya siasa, mtenda haki na uadilifu na mtu makini). Bodi haijawahi kufutwa na RITA na mara zote imeendelea kupokea malipo ya kisheria kuhusu usajili huo na kutoa Risiti. Mara ya mwisho Bodi ya wadhamini ya CUF imelipiwa kwa RITA Mwezi May mwaka 2016. Ni kwa msingi huo kuendelea kuifanya Bodi kuwa halali na iliyo Hai. Hivyo haiwezi kuisha muda wake kwa sababu Bodi ya wadhamini ya CUF haikusajiliwa kwa kipindi au kwa muda maalum (temporary registration), mathalani isemwe kuwa mwisho wake mwaka 2016, hapana na hilo haliruhusiki kisheria. Bodi ya wadhamini ya CUF uwepo wake ni wa kudumu (permanent registered body). Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa CUF wote wapo kwa mujibu wa sheria na wamechaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na imeelezwa ndani ya katiba ya CUF katika sura ya nane Ibara ya 98(1-6) hawateuliwi na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama na au Msajili wa vyama vya siasa.
Muda wa wajumbe hao haujaisha (expire), hakuna mjumbe aliyejiuzulu au kufariki hadi sasa. Wapo wajumbe watatu (3) kati ya hao wajumbe halali tisa (9) ambao hawajahudhuria vikao halali vya Bodi kwa sababu zisizofahamika rasmi na mamlaka iliyowateua. Kwa mujibu wa katiba ya CUF akidi ya kikao ni zaidi ya nusu ya wajumbe halali wa kikao husika.
Kutokuhudhuria kwao hakufanyi Bodi ya wadhamini iliyosajiliwa na RITA kwisha muda wake au maamuzi ya Bodi kuwa batili kwa sababu mara zote wajumbe sita (6) ambao ni zaidi ya nusu ya wajumbe halali waliopo wamekuwa wakihudhuria vikao na kutimiza akidi. Hata hivyo, CUF bado inawatambua kuwa ni wajumbe hao watatu (3) wasiohudhuria bado ni wajumbe halali wa Bodi ya wadhamini ya CUF na kinawasihi wahudhurie vikao vya Bodi ili watekeleze wajibu waliopewa na Chama. Tunataka wapotoshaji wafahamu kuwa; Bodi ya wadhamini na wajumbe wa Bodi hiyo kisheria ni mambo mawili tofauti. BODI NI TAASISI, BODI SIO WATU.
Hata kama Bodi ya wadhamini haitakuwa na wajumbe Bodi bado itakuwa hai na bado itakuwa na haki ya kumiliki au kuendelea kumiliki mali, inaweza kushtaki au kushtakiwa. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF haijagawanyika. Bodi ni moja pekee iliyosajiliwa RITA Mwezi May, 1993. Mali za chama zipo chini ya Bodi ya wadhamini na usimamizi wa kila siku wa mali hizo upo chini ya Katibu Mkuu ambaye kwa sasa ni Maalim Seif Sharif Hamad.
Hivyo Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini na wajumbe wake wapo karibu mno katika utekelezaji wa majukumu yao. Katibu Mkuu ndiye mwenye jukumu la kufanya mawasiliano ya kitaasisi ndani na nje ya chama kwa masuala yote (All correspondence should be done to Secretary General (Maalim Seif Sharif Hamad) through address…..) Na makhsusi kuhusu masuala yote yanayohusiana na mali za chama, kupokea na au kukabidhiwa mali za chama kabla ya kuwekwa chini ya wadhamini. Hata Msajili wa vyama vya siasa nchini anapotoa ruzuku anawasiliana na Katibu Mkuu na Serikali kupitia CAG inafanya kazi na Katibu Mkuu kukagua hesabu za chama na sio Mwenyekiti wa Chama au Bodi ya wadhamini. Tunapenda kuchukua fursa hii kuwajulisha wanachama wetu na watanzania kwa ujumla kupuuza taarifa za upotoshwaji zinazotelewa na watu wenye nia ovu na Chama.
3. KUHUSU KUFUNGWA KWA AKAUNTI ZA CHAMA NGAZI ZA WILAYA, KATA NA MATAWI NCHINI:
Wiki hii iliripotiwa kuhusu baadhi ya viongozi wa wilaya kulalamikia hatua ya kufungiwa kwa Akaunti zao za wilaya. Bodi ya wadhamini ya CUF yenye wajumbe toka pande zote mbili Bara na Visiwani imechukua uamuzi wa kuzifunga kwa muda (Temporary suspend) akaunti zote nchini Tanzania Bara na Zanzibar kwa ngazi ya wilaya, kata na matawi ya chama kutokana na wizi wa fedha za ruzuku uliofanywa na Lipumba na wenzake wakishirikiana na Msajili wa vyama vya siasa Jaji Franscis Mutungi. Nyote mnafahamu kuwa kwa mujibu wa katiba ya CUF ukurasa wa 85 Ibara ya 93 (1) (a-k) (2) imempa Katibu Mkuu wa Chama majukumu ya kuhakikisha kuwa; “Atakuwa Mtendaji Mkuu wa Chama na pia mwajibikaji mkuu wa shughuli zote za utendaji za Chama kitaifa” pia "Atakuwa mwajibikaji mkuu wa mambo yote ya fedha na mali za Chama katika ngazi ya Taifa (Chief Accounting Officer)” hatua hiyo ni sahihi ili kulinda mali za chama.
Tunawasihi viongozi wetu wasikubali kutumika kuhalalisha wizi huu kwa kugawiwa sehemu ndogo ya mamilioni ambayo taarifa zilizopo ni kuwa fedha hizo kwa kiasi kikubwa zimekwenda katika mgao wa matumizi binafsi ya waliofanikisha wizi huo. Ni matumaini yetu kuwa mara baada ya kukamilika kushughulikiwa kwa suala hili na ruzuku kurejeshwa katika utaratibu wa kikatiba akaunti hizo zitafungiliwa na kutumiwa fedha za wilaya zenu kama ilivyokuwa hapo awali.
Wito wetu tuendelee kuwa na subira wakati chama ngazi ya Taifa inashugulikia changamoto hizi zilizopandikizwa na wale wasiokitakia mema chama chetu. Viongozi wa Chama Taifa watafika katika wilaya zenu ili kujadiliana na kuelimishana zaidi juu ya masuala yote yanayoendelea ndani ya chama chetu. Bodi ya Wadhamini ya CUF Tayari imeshakamilisha taratibu za mashtaka juu ya wizi huo na kuyafikisha kwa mamlaka husika kwa hatua. Tutawajulisha zaidi wiki hii inayokuja.
4. KUHUSU UJENZI NA UIMARISHAJI WA CHAMA MAENEO MBALIMBALI YA NCHI:
Kurugenzi imepokea taarifa za viongozi na wanachama wetu kuendelea kukitumikia Chama chao bila kuchoka wala kukatishwa tamaa na mgogoro uliopandikizwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini ndani ya CUF. Viongozi wa wilaya za Mikoa ya Kusini, Pwani, Tanga, Nzega- Tabora, Kagera, Mwanza, na kwingineko wameendelea kufanya vikao vya kikatiba na uhamasishaji wa Chama, na kupongeza maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kukisimamia chama vyema na hatua wanazozichukua kukabiliana na uharibifu unaokusudiwa kufanywa na baadhi ya watu kwa kutumiwa na serikali ya CCM.
Aidha, wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, Mbunge wa Temeke Mhe. Abdallah Mtolea ameendelea na Operesheni- OCT (Okoa Chama Temeke) Tangu ilipoasisiwa kwake terehe 12/12/2016. Msingi wa kuanzishwa kwa OCT ni baada ya kuona baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo kutumiwa na CCM kutaka kulivuruga Jimbo la Temeke linaloongozwa na Mbunge wa CUF na kupandikizwa kwa upotoshwaji wa taarifa juu ya masuala mbalimbali na hasa zinazohusiana na uvamizi wa Lipumba ndani ya CUF baada ya miezi 12 ya kujiuzulu uenyekiti kwa hiari yake. Mpaka sasa wamezitembelea kata 14 kati ya kata 24 zilizopo ktk wilaya hiyo.
Zaidi ya wanachama 650 wamefikiwa. Katika tathmini ya OCT iliyofanyika hivi karibuni imebainika kuwa; Wanachama wengi walikuwa hawajui ukweli wa mambo yanayoendele ndani ya CUF, Wanachama wengi wakongwe ambao ni waanzilishi wa CUF hawakubaliani na Lipumba na kundi lake na mambo wanayokifanyia Chama. Wanachama wanahitaji kikao/Mkutano mkubwa ambao utahudhuriwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif na tayari washaanza maandalizi.
Aidha, Wanachama wamerudi kuwa kitu kimoja ktk kukihami chama chao. Ziara hizo zimeleta mafanikio makubwa na hivyo tunazitaka wilaya zingine nchini ambazo hazijaanza programu mfano wa hii, kubuni njia za kuwafikia wanachama katika ngazi za matawi na kata ili kuimarisha umoja na kuijenga CUF kama Taasisi imara ya kisiasa nchini.
5. UCHAGUZI MDOGO WA MITAA NA VIJIJI LINDI MJINI;
Wana-CUF wilaya ya Lindi wameendelea na Maandalizi ya uchaguzi mdogo wa mitaa saba na baadhi ya vijiji na vitongoji utakaofanyika tarehe 12/3/2017 na kampeni za uchaguzi huo zitaanza rasmi tarehe 26/2/2017. Wanachama, wabunge na madiwani wa maeneo mbalimbali wameombwa kujitokeza kwenda kushirikiana na viongozi wetu wa wilaya katika kampeni na kutoa michango yao ili kufanikisha ushindi kwa CUF.
6. TAARIFA YA MSIBA WA KATIBU WETU WA WILAYA YA KIBAHA VIJIJINI NDUGU JUMA SUFIANI;
Chama chetu cha CUF kimepata msiba wa Katibu wa wilaya ya Kibaha Vijijini Juma Sufiani kilichotokea ghafla usiku wa tarehe 17/2/2017 nyumbani kwake mtaa wa Idirisa, Magomeni-Dar es salaam. Mazishi ya marehemu yamefanyika Kibaha siku hiyo ya Ijumaa. Kamati ya Uongozi ya Taifa Chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Julius Mtatiro na Katibu Mkuu, Maalim Seif wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo na kutuma salama za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wanachama na viongozi wote wa CUF wilaya ya Kibaha Vijijini kwa kuondokewa na Kiongozi wetu katika Chama.
Tunawashukuru viongozi wetu wote wa kata ya Mzimuni, Magomeni na Kiongozi wa Wabunge wa CUF Bi. Riziki Shaali(MB) kwa kuweza kuratibu msafara na shughuli nzima ya kumsindikiza ndugu yetu katika mazishi-Kibaha. Tunawatakia wote subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Tunamuomba Mwenye-Enzi Mungu amsamehe mapungufu yake na amuingize katika neema za milele kwa rehema zake. “Hakika sisi sote ni waja wa Mwenye-Enzi Mungu na kwake yeye pekee tutarejeshwa”
Mwisho:
The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kitaendelea kuwajuza juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea na kamwe hakiungi mkono Juhudi zozote za Serikali ya CCM zinazokiuka taratibu na sheria za nchi ikiwemo ukandamizwaji wa demokrasia, mapambano dhidi ya madawa ya kulevya ambayo pamoja na ukweli wa tatizo hilo kijamii yanaonekana kutaka kuchukua mkondo wa kuwahujumu wananchi, wafanyabiashara, wasanii, viongozi wa dini na wanasiasa wasiopendeza machoni mwa watawala. Tunahitaji nchi iwe na dira inayoeleweka na programu/mpango wa maendeleo ya kiuchumi unaojulikana wazi kwa watanzania na kuacha kuendesha nchi kwa matamko yasiyokwisha kila kukicha. Kama tulivyoahidi hapo awali kila Jumapili tutawapa mukhtasari wa matukio muhimu, taarifa na masuala mbalimbali yaliyojiri na kuratibiwa na Chama.
Tunawahakikishia wana-CUF na watanzania kwa ujumla kuwa viongozi wenu wote wa kitaifa wapo makini kufuatilia nyendo zote za maadui wa chama na Intelijensia ya Chama inafanyakazi kwa umahiri mkubwa usiku na mchana bila kuchoka. CUF itashinda njama na hila zote zinazopangwa dhidi yake.
CUF NI TAASISI IMARA YENYE VIONGOZI MAKINI
HAKI SAWA KWA WOTE
----------------------------------------------
MBARALA MAHARAGANDE
K/NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA- CUF TAIFA
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577
Post a Comment