Ads

MAALIM SEIF SHARIF HAMAD AMVIMBIA LIPUMBA ASEMA HAONI SABABU YA KUKUTANA NAYE, ASISITIZA CHAMA KITASHINDA 2020.



Na. Salim Bimani 
mwambawahabari
Leo Alkhamisi, tarehe 09 Februari, 2017 Katibu Mkuu wa The Civic United Front (Chama Cha Wananchi), Maalim Seif Sharif Hamad, ameendelea na ziara ya siku nne katika Wilaya saba za Mikoa mitatu Kisiwani Unguja. Ziara hiyo iliyoanza Jana asubuhi katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini-Unguja imelenga kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zake kwa madhumuni ya kuhamasisha uhai wa Chama na umuhimu wa viongozi hao kushiriki katika kutekeleza mikakati mbali mbali iliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama.

Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ameambatana katika ziara hiyo na Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi, Mh. Omar Ali Shehe, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mh. Salim Bimani, na Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Mh. Abdalla Bakar Hassan. Viongozi wengine waliokuwepo ni Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake (JUKECUF), Mh. Zahra Ali Hamad, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa CUF (JUZECUF), Mh. Ali Abdallah Ali, viongozi wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVICUF) wakiongozwa na Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mh. Faki Suleyman Khatib na Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Mh. Mahmoud Ali Mahinda.


Katika mazungumzo na ujumbe wake kwa viongozi na wanachama wa Wilaya ya Kati Unguja, na Wilaya za Kaskazini A na B,  Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na mambo mengine:  amewataka wanaChama wa CUF kushirikiana na viongozi wakuu wa CUF Taifa wanaotambuliwa na Baraza Kuu la Uongozi katika kukijenga na kukiimarisha Chama hicho. Na kwamba wasiwe na wasiwasi na maamuzi yao waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 kwa kukipa ushindi Chama cha CUF kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kuwa hayatapuuzwa na kuendelea kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa InshaaAllah haki yao itarejea "Nawahakikishia, tumepigana vya kutosha katika kuidai haki yenu na tumefikia hatua nzuri za kuweza kupata haki yenu..…hatua ya wananchi wa Zanzibar ya kukipa ushindi Chama cha CUF ni kutokana na Chama cha CCM kushindwa kuwaongoza Wazanzibari kwa misingi ya haki, usawa na demokrasia” alisema.

Akitilia mkazo wa madai ya kupatikana kwa haki ya Wazanzibari ya tarehe 25 October Naibu Katibu Mkuu Mh. Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa CCM hawatasahau kipigo walichokipata tarehe 25 October 2015.

Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad amegusia mgogoro wa uongozi wa Chama cha CUF uliotokana na hatua ya Profesa Lipumba kuamua kurudi katika nafasi ya uwenyekiti wa Chama hicho, na kusema watahakikisha wanapata ushindi. Amesema; Lipumba amejiuzulu mwenyewe hivyo hakuna hoja yoyote ya kisheria inayomuwezesha kurudi tena katika nafasi hiyo. Barua ya kujiuzulu kwake iliwasilishwa kwa wajumbe wa mkutano mkuu ambapo pia wajumbe hao walidhia kujiuzulu kwake.

Akijibu madai ya Profesa Lipumba ya kutopokea simu zake pindi anapompigia, Maalim Seif amesema madai hayo hayana ukweli wowote. Amesema kukumbuka kwake Profesa Lipumba alimpigia simu mara moja na alipoikuta alimpigia Lipumba lakini hakuipokea. "Ninachoweza kusema ni kuwa Profesa Lipumba alinipigia mara moja, na nilipoona simu yake mimi nikampigia lakini hakuipokea, Pia siku ya pili asubuhi nilimpigia tena simu na ikaita lakini hakuipokea. Madai yake si ya kweli. Hasemi kweli" aliongeza.

Hata hivyo amesema haoni haja ya kukutana na Profesa Lipumba na kuzungumza mambo ya Chama kwani yeye si mwanachama halali wa CUF kwa sasa. "Profesa Lipumba anadai tukakutane ili tukapange mikakati ya kukijenga Chama, yeye si mwanachama wa CUF tukakutane kuzungumza nini?" alihoji. Maalim Seif amesisitiza kuendelea na kufuata taratibu za kisheria ili kuhakikisha Chama hicho kinamaliza moja kwa moja mgogoro huo uliopandikwiza na CCM kwa kumtumia Lipumba. Amewataka wapenzi na wanachama wa CUF kuunga mkono jitihada mbali mbali zinazofanywa na Chama katika kupigania demokrasia ya kweli hapa nchini.

Maalim Seif Sharif Hamad ataendelea na ziara hiyo Jumapili asubuhi, tarehe 12 Februari, 2017 katika Wilaya ya Magharibi ‘A’ na baadae mchana wa siku hiyo Wilaya Magharibi ‘B’. atamaliza ziara hiyo ya siku nne kwa kuitembelea Wilaya ya Mjini, Jumatatu tarehe 13 februari, 2017. Baada ya kukamilika kwa ziara katika kisiwa cha Unguja, Katibu Mkuu na Msafara wake wataendelea na ziara katika kisiwa cha Pemba kuanzia tarehe 15 Februari hadi tarehe 24 Februari, 2017.  Pamoja na kufanya ziara na kuzungumza na viongozi wa Chama na Jumuiya zake, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad atafanya uzinduzi na uimarishaji wa waratibu wa Chama, uzinduzi wa ofisi za Chama na kuweka mawe ya msingi katika majengo ya Chama katika maeneo mbali mbali ya kisiwa hicho.

HAKI SAWA KWA WOTE

____________
SALIM BIMANI
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI
NA MAHUSIANO NA UMMA
MAWASILIANO: 0777 414 112 / 0752 325 227

No comments