Ads

TUME YA TEHAMA YAWAKUTANISHA VIJANA KUTENGENEZA MAZINGIRA YA UBUNIFU WA TEKNOLIJIA.

Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA – ICTC) imesema itaendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa vijana katika sekta ya TEHAMA, hatua itakayowasaidia kufanya ubunifu utakaosaidia kujenga uchumi imara na shindani katika kanda, Afrika na dunia kwa ujumla.

Akizungumza Januari 20, 2026 jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Tisa la TEHAMA (TAIC 2026) linalofanyika katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kuwa wakati umefika kwa vijana kuchangamkia fursa za kufanya bunifu mbalimbali katika sekta ya TEHAMA ili kuleta tija kwa taifa.

Dkt. Mwasaga amesema kuwa kongamano hilo kwa siku ya leo limewapa vijana fursa ya kusikilizwa changamoto zao, kueleza ujuzi wao katika TEHAMA, pamoja na kutoa ushauri utakaofanyiwa kazi.

Amebainisha kuwa sensa ya mwaka 2022 imeonesha kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 ni zaidi ya milioni 21, na kwamba asilimia kubwa ya vijana walioshiriki katika kongamano hilo wameonesha uwezo mkubwa katika masuala ya TEHAMA.

“Leo tumekuja kuwasikiliza vijana katika sekta ya TEHAMA, hususan changamoto zao na ushauri wao. Baada ya hapo tutafanya majumuisho na kuyafanyia kazi ili kutatua changamoto zilizopo,” amesema Dkt. Mwasaga.

“Kuna Chuo cha Teknolojia kinachojengwa jijini Dodoma. Pia tunaunda taasisi za kulinda taarifa binafsi katika uchumi wa kidijitali, taarifa za mtu ni rasilimali muhimu sana, kwani kulinda faragha umjengea mtu imani katika matumizi ya teknolojia,” amesema Dkt. Mwasaga.

Kwa upande wao, vijana walioshiriki kongamano hilo, akiwemo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mvumbuzi wa Rafiki AI, Bw. Kevin Erasto, amesema kuwa kongamano hilo limewapa fursa ya kukutana na wadau muhimu kutoka sekta mbalimbali, ikiwemo wawekezaji, ambao wanaweza kusaidia kuendeleza bunifu zao.

Amesisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sekta ya TEHAMA ili kusaidia programu na bunifu za vijana kukua, kuleta manufaa makubwa na kukuza kampuni changa.

“Changamoto zinazoturudisha nyuma ni pamoja na uhaba wa vifaa vya kisasa vya kiteknolojia, mifumo ya malipo ambayo ingeweza kutusaidia kupata mitaji, pamoja na marekebisho ya baadhi ya sheria, hususan kwa kampuni changa,” amesema Bw. Erasto.

Naye Bi. Happy Mirra amesema kuwa miongoni mwa mambo muhimu yanayopaswa kufanyika ni utekelezaji wa vitendo wa mipango iliyopo, pamoja na kuangalia fursa kwa mtazamo wa kimataifa ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Kongamano la mwaka huu la TEHAMA ambalo linafanyika kwa siku tano na leo ikiwa siku ya pili, linaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Mabadiliko ya kidijitali yanayochochea athari za kijamii na uvumbuzi wa kiteknolojia kwa taifa lenye mafanikio, haki, ujumuishi na kujitegemea.”

Kaulimbiu hiyo inaakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, ambayo imetambua mabadiliko ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya kijamii katika kuwezesha ujumuishi wa wananchi wote, uvumbuzi endelevu na kujitegemea kiuchumi.

No comments