Ads

TUME YA TEHAMA YASISITIZA MSINGI WA MAPINDUZI YA KIDIJITALI KUPITIA DIRA YA TAIFA 2050

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, ameiagiza Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA – ICTC) kuongeza juhudi katika kuimarisha usajili na uendelezaji wa wataalamu wa TEHAMA, pamoja na kuimarisha mifumo ya kusimamia na kusaidia kampuni changa bunifu ili bidhaa na huduma zao ziweze kuingia sokoni na kuleta tija.

Akizungumza leo, Januari 19, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Tisa la TEHAMA (TAIC 2026), Mhe. Kairuki amesema kuwa ili mabadiliko ya kidijitali yawe endelevu na yenye tija, ni lazima yaungwe mkono na sera pamoja na sheria zinazoendana na kasi ya maendeleo ya sekta ya TEHAMA.

 “Ninaziagiza Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuhakikisha zinawasilisha Wizarani taarifa za mifumo yao ya TEHAMA, zikieleza namna mifumo hiyo inavyosomana na mifumo mingine. Aidha, wabunifu wahakikishe wanazingatia matumizi sahihi ya mifumo na teknolojia zinazoibukia, ikiwemo Akili Unde (AI), ili kuepuka matumizi yanayokiuka maadili ya nchi yetu,” amesema Mhe. Kairuki.

“Nimefurahi kusikia kuwa jukwaa hili limetenga siku ya leo nzima kwa ajili ya Wanawake katika TEHAMA. Hatua hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kidijitali na uvumbuzi wa kiteknolojia,” ameongeza.

Mhe. Kairuki amesema kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika kuendeleza TEHAMA, na kupitia kongamano hilo wanapaswa kuhamasisha wasichana wengi zaidi kuchagua masomo ya TEHAMA, kuimarisha umahiri wa kidijitali, na kuweka mazingira rafiki ya kisera na kitaasisi yanayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali, hivyo kuchangia kujenga Taifa lenye haki, jumuishi na linalojitegemea.

Mkurugenzi Mkuu wa TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kujadili Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, ambayo imetambua mapinduzi ya kidijitali kama dereva muhimu wa maendeleo. Amesema wadau wanapata fursa ya kukaa pamoja kwa siku tano kujadiliana juu ya hatua wanazopaswa kuchukua ili kufikia malengo ya dira hiyo.

Dkt. Mwasaga ameongeza kuwa dira hiyo imeainisha mapinduzi ya kidijitali kuwa chachu muhimu ya kuharakisha maendeleo, hivyo kongamano hilo linatoa fursa ya kuwasikiliza wataalamu wa ndani na nje ya nchi, makampuni, pamoja na sekta ya umma na binafsi.

Amebainisha kuwa mapinduzi ya kidijitali yana nguzo tano, zikiwemo sera na ujuzi. Ujuzi huo umegawanyika katika ngazi tatu: ujuzi wa msingi unaopaswa kuwa kwa kila mtu, ujuzi wa kati unaojumuisha mafundi na wahandisi, na ujuzi wa juu unaohusisha watafiti wanaobuni na kuendeleza mifumo mbalimbali ikiwemo Akili Unde (AI).

Amesema kuwa nguzo nyingine ni usalama wa kidijitali, unaojumuisha ulinzi wa watu, usalama wa mitandao, ulinzi wa faragha na taarifa binafsi, pamoja na ulinzi wa walaji.

Amesisitiza kuwa kongamano hilo limeandaliwa mahususi kujadili Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050 na kuandaa wataalamu wa TEHAMA pamoja na wananchi wote wanaotumia mitandao katika shughuli zao za kila siku, jambo litakalosaidia utekelezaji wa dira.

Amesema kuwa ya leo  wamejikita katika mada ya Wanawake na TEHAMA, ambapo watajadili mafanikio, changamoto zilizopo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kufikia uchumi jumuishi. Siku ya pili itahusu vijana, huku siku ya tatu, nne na tano zikihusisha wataalamu wa TEHAMA pekee.

Aidha, Dkt. Mwasaga amesema kuwa katika uchumi wa kidijitali kila mtu anapaswa kushiriki na kupata fursa ya kutumia teknolojia za kidijitali kupitia huduma mbalimbali za mawasiliano.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mifumo, Huduma za TEHAMA na Uzingatiaji kutoka  Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Angelina Misso, amesema kuwa miongoni mwa majadiliano ya kongamano hilo ni kuangalia jukumu la wanawake katika kusukuma gurudumu la maendeleo, hususan katika maeneo ya ubunifu wa teknolojia na matumizi yake.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha wanawake wanakuwa mstari wa mbele katika matumizi ya TEHAMA kuanzia wakiwa katika umri mdogo mashuleni. Kupitia kongamano hilo, wanawake wanaonesha mchango na jitihada walizofanya katika sekta ya TEHAMA kwa manufaa ya Taifa.

Kwa upande wao, washiriki wa kongamano hilo, akiwemo Rehema John, wamesema kuwa ushiriki wao ni fursa muhimu ya kutoa michango yao na kujadiliana kwa kina ili kuhakikisha Taifa linapiga hatua za maendeleo.

Kongamano la mwaka huu la TEHAMA linaongozwa na kaulimbiu isemayo:
“Mabadiliko ya kidijitali yanayochochea athari za kijamii na uvumbuzi wa kiteknolojia kwa Taifa lenye mafanikio, haki, ujumuishi na kujitegemea.”

Kauli mbiu hiyo inaakisi dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050, ambayo imetambua mabadiliko ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya kijamii katika kuwezesha ujumuishi wa wananchi wote, uvumbuzi endelevu na kujitegemea kiuchumi.






No comments