Ads

ASASI ZA KIRAI ZATOA WITO KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOA NAFASI SAWA KWA WAGOMBEA

 



Na Mwandishi wetu   - Dar es Salaam

MUUNGANO wa Asasi za Wanawake na Watetezi wa Usawa wa Kijinsia – Tanzania zimetoa wito kwa vyombo vya habari kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake kuratibu midahalo,makala na mijadala inayojenga uelewa wa umma juu ya uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo ya Taifa



Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 23,2025 Jijini Dar es Salaam ,Mwanzilishi wa TAMWA,Rose Haji amesema Asasi hizo zinazotetea makundi maalum ikiwamo wanawake, watoto na vijana wanawake, wameungana kwa pamoja kuhimiza umma kuhusu ajenda muhimu ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi sambamba na kuhimiza ushiriki wa wanawake katika upigaji kura siku ya Oktoba 29 mwaka huu.


 Amesema kwamba ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ni miongoni mwa vipaumbele vya asasi za kiraia zenye mrengo wa jinsia. Kwa hiyo tunaamini wakiwapo viongozi wanawake, kutakuwa na  hatua bymahsusi katika kuongeza kipato na maendeleo ya mwanamke. 


Aidha, amesema kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo zimepiga hatua katika ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi


"Tanzania imepata kiongozi mkuu wa nchi mwanamke, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye pia anawania kiti hicho cha urais kwa tiketi ya CCM na  mwaka huu kumekuwa na wagombea wengine wanawake wa urais, akiwemo Saumu Rashid kutoka UDP na Mwajuma Mirambo –UMD.Kwa upande wa  wagombea wenza wa urais kutoka vyama vingine ni pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR), Husna Mohamed Abdallah (CUF), Aziza Haji Selemani (D. MAKINI), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA).Hii ni hatua kubwa ya kidemokrasia kwa Tanzania na kwa ajenda ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.",amesema  mwanzilishi Haji


"wote.Tunapenda kuikumbusha jamii kuwa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi, ni muhimu kuepuka lugha za kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi — hasa kwa misingi ya kijinsia. Badala yake, mjadala wa kisiasa ujikite katika sera, ilani, na hoja zenye kujenga taifa",amesema Haji


Hata hivyo, amesema kuwa wanawake  waliowania nafasi ya udiwani hadi urais, wasibezwe, wasitukanwe, na tunakemea vikali lugha dhalili zinazotweza utu kwa wanawake wanasiasa na viongozi wengine wanawake


"Bado tunaamini  kwamba kumpata Rais mwanamke  Tanzania  imepiga hatua kubwa kupitia yeye katika kutekeleza Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) inayosisitiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika maamuzi.Kupitia Rais huyu mwanamke tumeona sheria kadhaa zikibadilishwa ikiwamo ya vyama vya siasa na hata miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya afya", 



Sanjari na hayo ,ameeleza Asasi za kiraia zinasimama imara katika kuhakikisha kuwa mafanikio haya yanaendelezwa, si kwa maneno tu bali kwa vitendo. Ushiriki wa wanawake katika siasa unaongeza uwajibikaji, uwazi, na ustawi wa kijamii, kwa kuwa tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanawake viongozi wanapendelea sera zinazogusa elimu, afya, haki za watoto, na usawa wa kiuchumi. Kama zipo changamoto kupitia uongozi wake basi si muda wa kumkashifu kwa kupitia jinsia yake.


Aliendelea kwamba  tunaikumbusha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa, na wadau wote kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanakuwa salama, jumuishi, na huru dhidi ya vitisho, udhalilishaji, na ukatili wa kijinsia, ambao mara nyingi huwakatisha tamaa wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa.

No comments