Ads

WAZIRI MKUU ATOA PONGEZI UWEKEZAJI SEKTA YA HALI YA HEWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya sita imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya Hali ya Hewa ikiwemo kufunga miundombinu ya kisasa ya hali ya hewa.

Akizungumza leo Aprili 25, 2024 Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya Serikali Bungeni kuhusu changamoto za hali ya hewa nchini, Mhe. Majaliwa amesema kuwa serikali imekuwa ikitoa mafunzo kwa watumishi kwa kuzingatia vigezo vya Kitaifa, Kimataifa pamoja na kuweka mifumo ya uhakika wa ubora wa huduma.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaojumuisha ununuzi wa rada za hali ya hewa.

"Nitumie fursa hii kumpongeza Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya hali ya hewa na kuijengea uwezo nchi yetu na kuifanya kuwa kinara Afrika na nje ya Afrika katika masuala ya utabiri wa hali ya hewa" amesema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa kuna rada mbili zinakamilishwa kufungwa katika mikoa ya Kigoma, Mbeya huku rada nyengine mbili zikitarajiwa kufungwa Dodoma na Kilimanjaro mwishoni mwa mwaka huu.

No comments