Ads

MZUMBE WAFANYA UTAFITI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu (HSRC) kutoka Nchi ya Afrika Kusini wanafanya utafiti kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo.   

Akizungumza na mwandishi wetu Jijini Dar es Salaam, Msimamizi Mkuu wa Utafiti huo na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam Dkt. Francis Mwaijande, amesema kuwa lengo la utafiti ni kutafuta taarifa zitakazowasaidia watunga sera nchini kujua kuna changamoto gani na maboresho yanayopaswa kufanyika ili kuongeza usalama wa uzalishaji wa chakula.

Dkt. Mwaijande amesema kuwa utafiti huo utaangalia hali ya kilimo katika maeneo ya vijijini na mjini ili kujua athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika sekta ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

“Kumekuwa na changamoto katika mifumo ya uzalishaji wa chakula nchini ambazo zimetokana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini zipo tafiti nyingi zimefanyika na kuonesha matumizi ya teknolojia yanaweza kuwasaidia wakulima kuongeza kasi uzalishaji wa chakula” amesema Dkt. Mwaijande.

Dkt. Mwaijande amesema kuwa utafiti huo utafanyika kwa muda wa miezi mitatu katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Iringa pamoja na Njombe.

“Kuna timu ya watafiti kutoka Afrika kusini na Tanzania tayari wamejengewa uwezo jinsi ya kukusanya taarifa za utafiti ambazo zitakwenda kuwa msaada kwa watunga sera kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa” amesema Dkt. Mwaijande.

Ameeleza kuwa utafiti unakwenda kuangalia katika maeneo   tofauti hasa usalama wa chakula upande wa lishe, uzalishaji pamoja na upatikanaji.   

Dkt. Mwaijande amefafanua kuwa pia utafiti utaangalia kwa namna gani mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuongeza fursa au hasara katika uzalishaji wa chakula.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuleta mvua nyingi au upungufu wa mvua, ukiangalia kilimo chetu kinategemea mvua, ikitokea kuna upungufu wa mvua uzalishaji wa chakula unakuwa mdogo na kusababisha kupungua kwa usalama wa chakula” amesema Dkt. Mwaijande.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a, ametoa wito kwa mamlaka mbalimbali nchini kuchukua taadhari kuhusu kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinazoweza kujitokeza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka Dkt. Chang’a amesisitiza umuhimu wa sekta mbalimbali kuchukua taadhari ikiwemo kilimo na usalama wa chakula.

Amesema kuwa kutakuwa na vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao na miundombinu ya kilimo, huku akibainisha kuwa magonjwa kama ukungu (fungus) yanatarajia kuongezeka na kuathiri mazao kama nyanya, ufuta, maharage na mazao ya jamii ya mizizi.

“Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko wa upotevu wa rutuba pamoja na kuchukua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu wa masika” amesema Dkt. Chang’a.

Pia, ameshauri kuimarisha miundombinu ya kilimo hususani maneo ya mabondeni pamoja na kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza, huku akiwakumbusha wauzaji na wasambazaji wa pembejeo za kilimo kuhakikisha zinapatikana kwa wakati.

Kutokana athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Tanzania, utafiti unaofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Baraza la Utafiti wa Sayansi ya Binadamu (HSRC) kutoka nchi ya   Afrika Kusini utasaidia kwa asilimia kubwa katika kutunga na kufanya maboresho ya wa sera ili kupata majibu rafiki ya kuzuia athari zinazoweja kujitokeza.

Hivi karibuni Taifa limeshuhudia athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa baada ya kutokea mafuriko katika mikoa mbalimbali nchini na kuleta maafa pamoja na kuharibu miundombinu ya uzalishaji wa chakula.

Licha ya changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa nchini uzalishaji wa chakula umekuwa ukiongezeka kila mwaka.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema kuwa uzalishaji wa chakula nchini umeongezka kutoka tani milioni 17.4 kwa mwaka 2022 hadi kufikia tani milioni 20 kwa mwaka 2023.

 

No comments