Ads

DKT. GWAJIMA AONESHA NIA KUFANYA KAZI NA MEWATA KUTOA ELIMU KWA JAMII

Na Francis Peter 

Serikali imesema ipo tayari kufanya kazi na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) katika kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu afya ya Mwanamke 

Akizungumza leo Aprili 21, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa MEWATA uliofanyika katika hoteli ya New Afrika, 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Vikundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa wakati umefika wa kuongeza nguvu katika jitihada za kukabiliana na mila na desturi kandamizi katika jamii.

Dkt. Gwajima amesema kuwa MEWATA wanapaswa kufanya kazi na wizara katika kuhakikisha wanatengeneza misingi imara ya watoto wa kike kwa kupata afya bora ili waweze kufanya vizuri na kuleta ushindani.

Dkt. Gwajima amesema kuwa ni vizuri kuweka mikakati ya kuendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuwawezesha wanawake kupata huduma za afya na kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Ni muhimu kufanya kazi kwa ushirikiano katika utoaji wa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia kwa kuwezesha ujenzi wa vituo vya wanawake pamoja na vituo vya ushauri nasaha kwa walionusurika“ amesema Dkt. Gwajima.

“Jamii zetu bado zinakabiliwa na changamoto ya mila na desturi kandamizi ambazo zinazowazuia wanawake na watoto kufikia ndoto zao na kutoa mchango wao katika ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla“ amesema Dkt. Gwajima.

Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) Dkt. Zaituni Bokhary, amesema kuwa kuna changamoto nyingi zinawapata wanawake lazini wanashindwa kusema kutokana na mila potofu zilizopo kwa baadhi ya jamii.

Dkt. Bokhary amesema kuwa ili kufika malengo tarajiwa wamejipanga kutoa elimu kuhusu afya ya mwanamke katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo vijijini.

“Tupo tayari kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuweka mipango rafiki katika kuhakikisha tunawafika walengwa na kuwapatia elimu hasa maeneo ya vijijini ambapo kunaonekana kuna uhitaji mkubwa” amesema Dkt. Bokhary.

No comments