RC RUKWA AZUNGUMZIA NA MIMBA ZA UTOTONI KWA WANAFUNZI
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joseph Mkirikiti akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Kirando wilaya ya Nkasi kwenye moja ya ziara zake kuhamasisha elimu .
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba akiongea kwenye kikao cha skauti na Mkuu wa Mkoa jana mjini Sumbawanga ambapo alisema atakashirikiana nao kutoa elimu ya kuchukia vitendo viovu ikiwemo rushwa na mimba za utotoni.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameagiza Wakuu wa Wilaya za mkoa huo
kuhakikisha wanafuatilia na kudhibiti kuongezeka kwa wanafunzi wa kike
wanaokatisha masomo kutokana na tatizo la mimba.
Akizungumza
juzi (19.11.2021) mjini Sumbawanga Mkuu huyo wa Mkoa alionesha kutofurahishwa
na kasi ya kuongezeka kwa wanafunzi wa kike wanaoshindwa kukamilisha masomo yao
sababu ikitajwa kuwa ni kupata ujauzito.
“Lazima
tuongeze mapambano kudhibiti mimba za utotoni .Sijafurahishwa kuona wilaya ya
Nkasi ikiwa na idadi ya wanafunzi Ishirini Tano (25) mwaka huu waliopata mimba
wakiwa wanasoma. Hii haikubaliki. Wakuu wa wilaya nendeni mkadhibiti vitendo
hivi” alisisitiza Mkirikiti.
Takwimu
za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa zimeonesha kuwa katika mwaka huu 2021 wilaya ya
Nkasi imekuwa na matukio 25 ya wanafunzi wa kike kupata mimba huku wilaya ya
Kalambo ikiripoti wasichana wanane (8) na Wilaya ya Sumbawanga nayo ikiwa na wanafunzi
wanane (8).
Mkirikiti
aliagiza pia Maafisa Elimu Kata kutimiza majukumu yao kwa kufuatilia walimu na
watu wanaojihusisha na kuwapatia mimba wanafunzi kwani zipo taarifa baadhi ya
walimu wanahusika na vitendo hivyo kinyume na maadili ya kazi.
“Maafisa
Elimu Kata mmepewa pikipiki na serikali ili zitumike kutekeleza majukumu ya
kusimamia elimu kwenye mashule ikiwemo kufuatilia wazazi na walezi wasiolea
watoto wao hatua inayopelekea baadhi ya watoto wa kike kupata mimba na watoto
wengine kuacha shule bila sababu” alisitiza Mkirikiti.
Aidha, Mkirikiti amemwagiza Afisa Elimu Mkoa
wa Rukwa Samson Hango kuhakikisha timu anayoingoza inajipanga kuchukua hatua
kali za kinidhamu na kisheria kwa walimu wote wanaoshabikia mimba za utotoni
kwenye maeneo yao.
Katika
hatua nyingine Mkirikiti ameagiza vijana wa skauti kote mkoani Rukwa kutumika
na halmashauri kubaini wazazi wanaotekelekeza watoto na kusababisha wahamie
mitaani na kuitwa ’watoto wa mtaani’ ambao wanazidi kuongezeka hususan Manispaa
ya Sumbawanga.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema atahakikisha
anashirikiana na vijana hususan skauti kufundisha vijana umuhimu wa maadili
mema ili waweze kuwa raia wema na kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.
Waryuba
aliongeza kusema jamii inatakiwa kuelimishwa juu ya umuhimu wa uzalendo hatua
itakayosaidia kuwa na jamii bora itakayochukia maovu ikiwemo rushwa.
Mwisho.
Post a Comment