SERIKALI YAKANUSHA KUPORWA ARDHI YA WANANCHI NA VIONGOZI WA UMMA
Mwambawahabari
Na Munir Shemweta, WANMM DAR ES SALAAM
Serikali imekanusha taarifa
ya kuporwa ardhi ya wananchi na viongozi wa umma kilichokuwa kiwanja NA 11 Eneo
la Ununio katika Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam kama ilivyosambaa kwenye
mitandao ya kijamii.
Akikanusha kuporwa kwa
eneo hilo leo jijini Dar es Salaam mbele wa waandishi wa Habari, Katibu Mkuu
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema taarifa
zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kuporwa kwa eneo hilo siyo
za kweli kwa kuwa eneo hilo lilishabatilishwa kwa mujibu wa fungu la 48 (3) la
sheria ya ardhi Na 4 (1999).
Makondo aliwaasa wananchi
kuipuuza taarifa hiyo kwa kuwa ina lengo la kuwachafua viongozi na kubainisha
kuwa, kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 4 (1999) Kamishna wa Ardhi anayo mamlaka
kisheria kumilikisha ardhi kwa Mtanzania yoyote aliyetimiza masharti kisheria.
Akifafanua kuhusiana na
suala hilo Kamishna wa Ardhi Nchini Mathew Nhonge alisema eneo linalodaiwa
kuporwa lilipimwa kwa mara ya kwanza mwaka 1988 na kuitwa kiwanja namba 11 eneo
la Ununio.
Nhonge alisema, mwaka
1988 Manispaa ya Kinondoni ilimilikisha kiwanja hicho kwa Ndg Goodfreid Kajana Makaya na kupewa Hati NA 43711 ambapo
baadaye kulijitokeza malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wakidai kuwa ni
wenyeji wa eneo hilo akiwemo Ramadhani Mwinyihamisi, Waziri Kibosha na Bi
Kijakazi Maulid.
Kamishana huyo wa Ardhi
nchini alibainisha kuwa, malalmiko hayo yalisababisha mgogoro uliofikishwa
Makahakama kuu Kitengo cha Ardhi kupitia
Shauri la Ardhi NA 93/2004 baina ya Bi
Kijakazi Maulid dhidi ya mmiliki halali Ndg Goodfreid Kajana Makaya ambapo hata
hivyo shauri hilo lilitupiliwa mbali na Mahakama hiyo baada ya Bi. Kijakazi
kushindwa kuthibitisha madai yake.
Nhonge aliongeza kwa
kusema, mwaka 2007 Ndg Goodfreid Kajana Makaya alihamisha umiliki wake kisheria
kwa kuiuzia Kampuni ya Shamiana Builders Limited aliyoieleza kuwa nayo ilishindwa
kutekeleza masharti ya uendelezaji kama ilivyoelelekezwa kwenye hati miliki na
hivyo kusababisha haki ya umiliki kufutwa mwaka 2017 na serikali kwa mujibu wa
fungu la 48 (3) la sheria ya ardhi Na 4 (1999).
Kufuatia hali hiyo,
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ililipanga na hatimaye
kulipima upya eneo hilo na takribana viwanja 22 vilipatikana na kumilikishwa
kwa wananchi mbalimbali wakiwemo wakazi wa Uninio ambao maombi yao ya kumilikishwa
yaliwasilishwa serikalini.

Post a Comment