MWAKALINGA ATOA SIKU MBILI BARABARA KUKARABATIWA
Mwambawahabari
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia
Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amemuagiza Meneja wa
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mbeya, kuhakikisha
ndani ya siku mbili anakarabati maeneo yote korofi yaliothiriwa na mvua
katika barabara ya Isyonje- Makete (Km 96.4) ili iweze kupitika majira
yote ya mwaka.
Mwakalinga,
ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati alipokuwa akikagua athari za mvua
katika miundombinu ya barabara hiyo inayounganisha mkoa wa Mbeya na
Njombe akiwa katika kijiji cha Igoma, ambapo amesema kuwa barabara hiyo
ni muhimu kwani ni kiungo cha mawasiliano kati ya mikoa hiyo miwili.
“Hakikisha
Meneja, barabara hii inapitika ifikapo kesho, kusanya wataalamu wako
wote waliopo katika mkoa wako, mje hapa kufanya kazi ili kuhakikisha
barabara hii inarudi katika hali yake ya awali” amesema Mwakalinga.
Amesisitiza
kuwa licha ya mvua kuendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo lakini
bado wananchi wanahitaji hali nzuri ya barabara ili kurahisisha huduma
za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao kutoka sehemu mbalimbali.
Mwakalinga,
amefafanua kuwa ameamua kufanya ziara hiyo ili kubaini athari za mvua
katika miundombinu ya barabara na kutatua changamoto zake pamoja na
kuangalia maendeleo ya miundombinu hiyo katika maeneo mbalimbali nchini
ili kuzipa kipaumbele katika kuzitengea fedha barabara zote zenye
changamoto kwenye bajeti ijayo.
“Kama
mnavyojua kipindi cha bajeti kimekaribia, sasa ni muhimu kuzikagua
barabara hizi ili nione namna ya kuzipa kipaumbele kwa kuziwekea fedha
katika bajeti ijayo kwa barabara zote ambazo zina changamoto”,
amefafanua Mwakalinga.
Kwa
upande wake, Meneja Wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Eliazary
Rweikiza, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa atakarabati kwa wakati
barabara hiyo na kuhakikisha inapitika majira yote ambapo ameongeza kuwa
tayari mkandarasi ameshaaanza kurekebisha sehemu zilizoharibika na
kwamba ndani ya siku mbili kazi zote zitakuwa zimekamilika na barabara
kupitika.
Katika
hatua nyingine, Mwakalinga, amekagua barabara ya Njombe- Ndulamo –
Makete sehemu ya Moronga – Makete (Km 53.5) ambayo inajengwa kwa kiwango
cha lami na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group.
Mwakalinga,
amemtaka Mkandarasi huyo kuendelea na ujenzi kwa kazi ambazo zinaweza
kufanyika katika kipindi hiki cha mvua ili mradi ukamilike kwa muda
uliopangwa kulingana na mkataba.
Naye,
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusufu Mazana,
amemhakikisha Mwakalinga kuwa atamsimamia mkandarasi huyo ili aweze
kukamilisha kwa wakati kwani mradi huo ni muhimu katika usafirshaji wa
mazao ya misitu, chakula pamoja na utalii.
Post a Comment