Ads

SERIKALI YATUMIA MFUMO MPYA WA TEKNOLOJIA KUNUNUA KOROSHO.

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeabadili mfumo wa ununuzi wa korosho kwa mwaka 2019/ 2020 baada ya kutangaza kutumia mfumo mpya wa teknolojia kwa wanunuzi kujisajili kwenye Bodi ya Korosho kupitia mfumo wa Wizara ya Kilimo wa kusimamia Biashara za Kilimo (Agricultural Trade Management Informataion System – ATMIS).

Hatua hiyo imekuja baada ya mwaka wa jana kuwa na changamo katika bei ya korosho, jambo ambalo serikali iliamua kuingilia kati kwa kununua korosho zote kwa wakulima ili kuhakikisha wananufaika na zao hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga, amesema kuwa msimu wa mwaka 2019/2020 mfumo wa ununuzi wa korosho utakuwa kwa njia ya mnada wa wazi kwa kutumia jukwaa la Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) ambapo hakutakuwa na matumizi ya masanduku ya mnada kama ilivyokuwa awali.

Mhe. Hasunga amesema kuwa wanunuzi watakaosajiliwa watatakiwa kulipa kinga ya dhamana (Bid Security) kwa kutegemeana na kiasi cha korosho ambacho mnunuzi amekusudia kununua kupitia akaunti ya usuluhishi inayomilikiwa na soko la bidhaa.

“Mfumo huu utaruhusu wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani kushiriki katika mnada, wanunuzi wa nje ya nchi wataweza kushiriki katika mnada kitu ambacho kitakuwa na tija katika zao la korosho” amesema Mhe. Hasunga.

Ameeleza kuwa wanunuzi hao watadhaminiwa na benki za malipo (Settlement Bank) zinazotambuliwa na soko la bidhaa (TMX) kitu ambacho kitasaidia kuongeza ushindani katika minada.

“Benki za malipo zitawajibika kutoa uhakikisho wa uwepo wa fedha kwa ajili ya malipo ya korosho kwa mujibu wa taratibu za soko,”amesema Mhe. Hasunga. 

Hata hivyo amefafanua kuwa septemba 30 mwaka huu kutakuwa na mkutano na wadau wa korosho hapa nchini ili kuwaeleza namna ya utaratibu ulivyo wa ununuzi wa korosho.

Katika hatua nyingine ameeleza kuwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi awataruhusiwa kununua korosho ghafi kwa mafungu (stakes) kati ya tani 50 mpaka tani 500 kulingana na mahitaji.

“Korosho hizo katika mafungu (stake) zitapangwa kulingana na vigezo vya ubora na daraja,  kiwango cha korosho kitakachouzwa katika kila (mnada) kitatokana na taarifa zilizopo katika katalogi ya mauzo,” amesema Mhe. Hasunga.

Amesema kuwa mnunuzi atalazimika kununua kiasi chote cha korosho kilichopo katika fungu katika mnada ili kuwezesha utoaji wa korosho katika ghala kwa kutumia utaratibu wa korosho za kwanza kuingia ndizo za kwanza kutoka (first in, first Out- FIFO).

Wanunuzi wenye leseni watapewa msimbo (code) maalumu watakazozitumia kuingia kwenye mfumo na kushiriki katika minada, huku mnunuzi atakaeshinda katika mnada atawajibika kulipia korosho alizoshinda ndani ya siku tatu (3) baada ya mauzo kufanyika.

Amesema kuwa malipo yote yatafanyika kupitia benki za malipo (Settlement Bank) zinazotambuliwa na soko la bidhaa, soko la bidhaa litawalipa wadau wote kwa mujibu wa sheria ndani ya siku mbili tangu mnunuzi kukamilisha malipo husika.

“Minada ya mauzo ya korosho itafanyika siku mbili kwa wiki katika maghala yote kulingana na upatikani wa korosho, minada itakuwa siku ya Jumanne na Alhamisi,” amesema Mhe. Hasunga.

Mhe. Hasunga amesema lengo la utaratibu huu mpya ni kupanua wigo wa soko ambao wanaamini utaongeza chachu ya ushindani na kuwezesha bei nzuri zaidi kupatikana kulingana na mwenendo katika soko la dunia.

Kupitia jukwaa la soko la bidhaa kutakuwa na wigo mpana kwa wanunuzi, kutakuwa na uwazi wa bei za korosho na wakulima watalipwa haraka zaidi na kwa wakati.

Alisema lengo la Serikali ni kuona wakulima wote wanalipwa fedha zao moja kwa moja  kwenye akaunti zao binafsi katika Benki zilizopo katika maeneo yao ya uzalishaji.

Alibaiisha kuwa Wizara ina mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji ikiwa ni pamoja na Kuhamasisha matumizi sahihi ya viutilifu bora na  kuhakikisha upatikanaji wa viuatilifu hivyo kwa wakati na kwa bei nafuu pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima.

Ameeleza kuwa  matumizi sahihi ya viuatilifu yataongeza tija miongoni mwa wakulima kutoka wastani wa kilo 10 kwa mti kwa mwaka hadi kufikia kilo 35 kwa mti kwa mwaka.

Wizara kupitia Bodi ya korosho imeongeza maeneo mapya yanayolima korosho kutoka mikoa mitano ya awali ambayo ni Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga na kufikia mikoa 17.

“Mikoa mingine inayolima korosho kwa sasa ni Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Katavi, Morogoro, Songwe,Kigoma, Njombe na Shinyanga,”amesema Mhe. Hasunga.

 Lengo la Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. John Magufuli ni kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na mazao yao na kupata bei nzuri kulingana na mwenendo wa soko.

Imeeleza kuwa kuhusu deni la korosho msimu uliopita  inalodaiwa na wakulima wakubwa shilingi bilioni 50, ambalo linaendelea kulipwa kila siku kulingana na shehena ya korosho zinazonunuliwa na wanunuzi.  

No comments