Ads

Makonda apokea Msaada kutoka kwa Balozi wa UAE kusomesha watoto wa kike 100

 
Hussein Ndubikile
Mwambawahabari
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amepokea msaada wa kuwasomesha watoto wa kike 100  waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano mwaka huu wanaochukua masomo ya sayansi  kutoka kwa Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE),Khalifa Abdulrahiman Almazouqi.

Wanafunzi waliopatiwa msaada unaojumuisha ada na vifaa vya shule ni wale waliobainika kuwa wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia masomo.
Akizungumza jijini humo mkuu wa mkoa huyo alisema ameamua kujitoa kwa dhati kuwasaidia watoto wa kike wanaochukua masomo hayo kwa kukumbuka alipotoka kwani alisaidiwa ndugu, jamaa na marafiki kufika alipo sasa.

“ Nimefika hapa si kwa uwezo tu wa wazazi wangu  bali nlisaidiwa na ndugu na marafiki hivyo ninao wajibu kukumbuka nilipotoka hadi nilipofika watoto mnaowaona wazazi wao hawana uwezo kuwasomesha,” alisema Makonda.

Alibainisha kuwa hata Rais Dkt. John Magufuli ameonyesha dhamira ya dhati ya kuwakumbuka wanyonge kwa kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne.

Alisisitiza kuwa Hayati Mwalimu Nyerere katika matamko yake alishawahi kusema ukombozi wa mnyonge unapatikana kwa kumpatia elimu hivyo hilo kauli hiyo imempa msukumo wa kuwasaidia watoto hao watimize ndoto zao.

Alifafanua kuwa watoto wa kike  wakipatiwa elimu wanapata heshima kwenye jamii kwani wanakuwa na uwezo wa kuchanganua mambo na kuchangia mambo katika ngazi ya familia.

Pia alisema ameonelea kuanza safari ya kuwasaidia watoto wa kike kwa kuangalia kigezo cha mazingira magumu na vishawishi wanavyokutana navyo na ugumu wa masomo hayo.

Vigezo vingine ni umuhimu wa sayansi wakati nchi ikielekea uchumi wa kati kupitia viwanda, kuzitafutia ufumbuzi wa wataalamu sekta ya madini na nishati pamoja na umuhimu wa kutengeneza wanasayani wengi wa kike nchini.

Aliwahimiza kuzingatia masomo yao ili weweze kulinda na kutimiza ndoto zao waje kulitumikia taifa katika miaka ya baadaye na kumshukuru balozi wa UAE.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lisu alisema msaada uliotolewa umewalenga watoto wa kike wenye wazazi wasiomudu gharama za masomo.

Alimshukuru na kumpongeza Makonda kwa mchango wake katika elimu kwani ameweza kufanikisha ujenzi wa ofisi 46 za walimu za kisasa lengo likiwa kufikisha 402 kwa michango ya wahisani.

Lisu alisema mkuu wa mkoa huyo ameshawasaidia walimu 800 kukopeshwa viwanja vya gharama nafuu huku akimpongeza kuweka utaratibu mzuri wa kuwasomesha watoto hao.

Naye Balozi wa UAE, Khalifa alisema ameamua kutoa msaada huo kwa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na kuwataka watoto hao kushikilia masomo watimize ndoto zao.
Alisema mradi huo ni wa mwanzoni na kwamba mbeleni watatoa msaada wa chakula kufanikisha masomo yao na kumshukuru Rais Magufuli kwa sera yake ya elimu bure.

Mzazi Anna Fundi alimshururu Makonda kwa kusaidia watoto hao kuweza kuendelea na masomo yao na kuwataka wazazi wenzange kumuombea ili aendelee kuwa na moyo  wa kusaidia.

Aliwasihi watanzania waache kubaguana badala yake wapendane kufanikisha Tanzania kuwa nchi iliyoendelea.

Mwanafunzi wa Kidato cha Tano wa Shule ya Sekondari Kisutu, Velaria Reuben alimshukuru Makonda kwa kuguswa na hali zao na kuahidi kutomwangusha katika masomo yao ili baadae waweze kusaidia wenzao wenye uhitaji.

No comments