Ads

Rais Magufuli Akutana na Viongozi wa Dini Ikulu Jijini Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali ya Kajamii.


 

Paschal Dotto-MAELEZO.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameshukuru sana viongozi wa dini kwa kumuombea katika utendaji kazi wa serikali yake ya Awamu ya Tano ili kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Nawashukuru sana ninyi viongozi wa Dini kwa kuendelea kuniombea mimi pamoja na watendaji wa Serikali yangu, lakini pia nilifikiri ni vizuri kuukaribisha mwaka kivingine kwa kujadili mustakabli wa nchi yetu kwamba, katika miaka 3 mumetupima vipi, lakini pia muweze kutoa ushauri ili tuweze kwenda sawa katika ujenzi wa nchi yetu”,  alisema Rais Magufuli
Mkutano huo uliohusisha viongozi wote wa dini kitaifa  na kuibua michango mbalimbali kutoka kwa Mashekhe, Maaskofu na Wachungaji kutoka Taasisi za kidini waliochangia na kuuliza maswali katika mkutano huo, huku Sekta za Elimu, Afya na Maji zikitawala kwa michango ambayo ilipata ufafanuzi kutoka kwa Rais John Pombe  Magufuli.
Akifafanua michango hiyo Rais Magufuli aliwathibitishia viongozi wa dini kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hoja zote zilizotolewa kwenye mkutano na iko pamoja na Taasisi za dini katika kuifanya Sekta ya Elimu, Afya na Maji kuwa bora zaidi kuwasaidia wananchi
“Napenda kuwathibitishia viongozi wote wa dini kuwa ushauri na michango yenu katika mkutano huu tumeichukua, kwa hiyo viongozi hawa 42 waliowakirisha wengine kutoa michango hii wamefanya jambo zuri sana na yote haya tutayachukua na kuyafanyia kazi ili kujenga nchi yetu”, Alisema Rais Magufuli.
Akifafanua michango iliyotolewa katika Sekta ya afya iliyotaka Taasisi za dini na Serikali kushirikiana bila kushindana katika ujenzi wa sehemu za afya kama vile zahanati, vituo vya afya na hospitali, Rais Magufuli alisema kuwa kuna Zahanati 791, vituo vya Afya 160, Hospitali 116 kutoka Taasisi za dini ambazo zinafanya kazi nchini kuwasaidia wananchi, pia Serikali imesaini mkataba na hospitali 92 za Taasisi za Dini ili kuweza kuzipatia vifaa tiba kwa kuongeza miundombinu rafika kwa matibabu kwa wananchi
Kwa upande wa Elimu Rais Magufuli alisema kuwa Serikali iliamua kuchukua hatua madhubuti katika kudhibiti ubora wa elimu nchini kwa kuvifungia baadhi ya Vyuo vya Dini ili kulinda thamani ya ubora wa elimu nchini, kwa ujumla Taasisi za dini zinamiliki shule za Msingi 347, shule za Sekondari 459, Vyuo vya Ufundi 228, Vyuo Vikuu 14 na  Vyuo Vikuu Vishiriki 12
“Natambua mamilioni ya watanzania wananufaika na elimu kutoka katika shule hizi lakini kusimamia ubora wa elimu ili kupata wasomi bora ni vizuri zaidi, Kwa sababu ilifikia mahara kila mmoja alitaka kuanzisha Chuo Kikuu na kudahili wanafunzi kutoka TCU, tulipoona kuwa kuna mapungufu kwenye ubora wa elimu ilibidi sisi kama Serikali tuingilie kati na kuamua kuvifungia baadhi ya vyuo vya elimu ya juu”, Alisema Rais Magufuli.
Katika Sekta ya Maji Rais Magufuli alieleza miradi inayofanyika ili kufanikisha upatikanaji wa maji kwa wananchi nchi nzima, huku akieleza sababu za kukwama kwa miradi mbalimbali ya maji iliyokwamishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali  walikuwa wanapeleka miradi hiyo harafu haikamili kwa kutokuwa waaminifu, lakini kwa sasa Serikali imeamua kuchukua juhudi madhubuti.
“Serikali inafanya juhudi kubwa kwa sasa kutekeleza  miradi mikubwa ya kuwapatia maji wananchi, kwa mfano Mradi wa maji Arusha ambao utagharimu shilingi Bilioni 520 na huu mradi utahudumia kwa asilimia 100 kwa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani kwa kuwa utakuwa na visima virefu 52, lakini pia mradi mkubwa kutoa ziwaViktoria- Nzega- Tabora- Igunga hadi Sikonge ambao utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 500, ujenzi wa miradi ya maji kwa Miji 27 nchi nzima utakaogharimu shillingi Trilioni 1.2 na mwisho kabisa miradi ya maji ya World banki kwa bilioni 800”, Alisema Rais Magufuli.
Aidha katika mkutano huo Rais Magufuli alizungumzia suala la demokrasia na kusema kuwa Tanzania kuna Demokrasia kubwa sana kwani hakuna mwanasiasa yeyote aliyezuiliwa kufanya mikutano jimboni kwake alikoshinda baada ya uchaguzi.
“Nataka niwahakikishie ndugu zangu kuwa Tanzania kuna demokrasia ya hali ya juu, kwani demokrasia siyo maandamano tu, watu wanajenga barabara wewe unaandamana, watu wanajenga hospitali wewe unaandamana, kwenye nchi zingine uchaguzi ukiisha wanaendelea na kazi ya kujenga nchi kwani wanajua bila amani mahali popote hakuna maendeleo, na demokrasia ina mipaka yake kwa hiyo hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano sehemu yake”, Alisisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliwashukuru viongozi wa dini kwa kutoa ushari kwa Serikali na kuwahakikishia kuwa ushauri walioutoa Serikali imeuchukua na aliwataka watendaji wake kufanya mikutano kama hiyo ili kutatua matatizo ya wananchi.

No comments