MGANGA MKUU SINGIDA APEWA WIKI MBILI KUBORESHA AFYA MAKAZI YA WAZEE
Mwambawahabari
Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo yaJamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na Wazee waishio Makao ya Wazee Sukumahela Wilayani Manyoni wakati wa ziara take inayoendelea Mkoani Singida.
.......................................................................
Na ANTHONY ISHENGOMA
Naibu
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt.Faustine Ndugulile amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida
kuhakikisha wazee wasiojiweza wanaoishi Makao ya Wazee ya Taifa
Sukamahela wanapatiwa vyandarua kwa ajili ya kujikinga na Malaria.
Naibu
Waziri Ndugulile ametoa agizo hilo alipotembelea makao hayo yaliyoko
nje kidogo ya mji mdogo wa Manyoni kujionea hali halisi ya maisha ya
Wazee wasiojiweza.
Dkt. Ndugulile ametoa muda wa wiki mbili kwa
Mganga Mkuu Mkoa kutekeleza jambo hilo na kutaka mrejesho wa utekelezaji
wa agizo hilo.
"Hili ni kosa ambalo siwezi kulisamehe tuna
vyandarua vingi vya kutosha sioni sababu wazee hawa kulala kwenye
vyumba bila vyandarua, nawapa wiki mbili kuhakikisha kila mzee analala
kwenye chandarua.," Aliagiza Dkt.Ndugulile.
Pia Dkt. Ndugulile
amewataka watendaji wa Idara ya Afya wa Zahanati ya Sukamahela iliyopo
katika eneo la makao ya Wazee hao kuhakikisha wanakuwa na dawa za
kutosha hasa zile maalumu kwa ajili magonjwa ya Wazee.
Makao ya
Wazee Sukamahela pamoja na mambo mengine yanayowakabili na upungufu wa
chakula, na wamekili kuchoshwa na ulaji wa aina moja ya mboga hivyo
kutoa ombi lao kwa Naibu Waziri kutatua changamoto hiyo.
Naibu Waziri Ndugulile amehaidi kushughulikia suala la ukarabati wa majengo chakavu ya yaliyopo katika Makazi hayo.
Kwa
nyakati tofauti wazee waishio katika makazi hayo wamelalamikia ukosefu
wa umeme katika makazi hayo, dawa za magonjwa ya ukoma na vifaa vidogo
vidogo kwa ajili ya usafi na kilimo cha mbogamboga pamoja na miundo
mbinu chakavu ya vyoo.
Aidha Dkt.Ndugulile amesema serikali
inakusudia kufunga baadhi ya vituo na kuvipanga kikanda ili iweze
kudumisha huduma kwa wazee wasiojiweza lakini kugeuza makazi
yatakayofungwa kuwa nyumba salama kwa ajili kupambana na vitendo vya
kikatili.
Naibu Waziri Ndugulile yupo mkoani Singida kufuatilia utekelezaji wa masuala ya Afya, Ustawi na Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo yaJamii,Jinsia,Wazee na Watoto
Dkt. Faustine Ndugulile akikagua Jiko kinapoandaliwa chakula cha Wazee
waishio Makao ya Wazee Sukumahela Wilayani Manyoni wakati wa ziara take
inayoendelea Mkoani Singida.a


Post a Comment