Halmasahuri Mkoani Rukwa zatenga milioni 79 kununua mbegu za kahawa.
Zao la kahawa ni miongoni
mwa mazao matano ya biashara ambayo serikali ya awamu ya tano imeamua kwa dhati
kutilia mkazo uzalishaji wake, kwa mkoa wa Rukwa zao hilo ndio zao ambalo
limeonekana kustawi kwenye baadhi ya maeneo na kupelekea halmashauri za mkoa
huu kutenga shilingi milioni 79 kwaajili ya kununua mbegu ili kuendeleza zao
hilo.
Mkuu wa Mkoa wa rukwa Mh.
Joachim Wangabo amesema kuwa kama mkoa hatuna budi kutilia mkazo uanzishaji na
uendelezaji wa zao hili ili wakulima wetu waweze kuwa na zao la biashara na
kubainisha kuwa tayari maeneo kwaajili ya kilimo hicho yameshabainishwa ambapo
makampuni, taasisi na wakulima wameonyesha nia ya kulima.
“Eneo la kiasi cha ekari
3,195.83 limebainishwa kwa ajili ya kulimwa zao la kahawa. Jumla ya wakulima
2,266 na taasisi 9 zitajihusisha katika uzalishaji wa kahawa. zikiwemo taasisi
za Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania.”Alisema.
Ameyasema
hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika mwezi huu
wa nane katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa ikijumuisha wadau mbalimbali wa
maendeleo, Wabunge, Madiwani, Viongozi wa dini na wataalamu wa Halmashauri na
sekretarieti ya mkoa.
Aidha, mbunge wa viti
maalum Mkoa wa Rukwa Mh. Aida Khenan amesema kuwa kilimo cha kahawa kinahitaji
wakulima wenye uwezo wa kifedha ambao katika mkoa wa rukwa wakulima hao hawapo
na kusisitiza kuwa wakulima wa mkoa huo wamezoea kilimo cha muda mfupi.
“kahawa inahitaji fedha na
muda, wakulima wetu wamezoea kilimo cha muda mfupi, watakaoweza kumudu kahawa
ni wale wenye uwezo, masuala ya madawa na kuhudumia hiyo kahawa, wataalamu wetu
wafanye utafiti watuambie zao lipi la kibiashara litaleta tija kwa wananchi
wetu hasa katika msimu huu wa kilimo,” Alisema.
Mh. Wangabo alieleza kuwa
mkoa umejipanga katika kuhamasisha kilimo cha zao la alizeti kama zao la
kibiashara kwani hali ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa hairidhishi na hivyo
kutoleta tija kwa wakulima.
“Hali ya uzalishaji wa zao la alizeti katika Mkoa
umebaki kuwa ni wastani wa gunia 6.5 za
kilo 65 kwa ekari sawa na tani 1.1 kwa hekta. Tija hii ni ndogo sana
ukilinganisha na tija iliyofanyiwa utafiti ya gunia 12-16 kwa ekari ambazo ni
sawa na zaidi ya tani 2.00 kwa hekta.” Alibainisha.
Serikali ya Awamu ya Tano
imeamua kutilia mkazo uzalishaji wenye tija wa mazao matano ya biashara ambayo
ni Korosho, Chai, Kahawa, Tumbaku na Pamba.
IMETOLEWA NA

Post a Comment