ZANZIBAR WAPEWA SOMO LA UWAJIBIKAJI KUKUZA UCHUMI.
Wapili kutoka kushoto ni RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akiomba dua.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi kuwajibika ipasavyo katika kufanya kazi za halali ili wapate manufaa katika maisha yao na kukuza uchumi wao na kuimarisha ustawi wa jamii.
Alhaj Dk. Shein ameyasema hayo leo katika hotuba yake ya Eid el Hajj aliyoitoa huko katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Kizimkazi, iliyopo Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika maelezo yake,Alhaj Dk. Shein alisisitiza kwamba lazima wananchi wawe tayari kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Alisisitiza kuwa wale wote aliowakabidhi dhamana ya kuziongoza Wizara, Idara na Taasisi za Serikali wanapaswa waongeze kasi katika kusimamia kazi na kuwasimamia wanaowaongoza kwa kuzingatia sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011 pamoja na kanuni zake za mwaka 2014
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutilia maanani suala la wananchi kufanya kazi kwa bidii katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 na Utekelezaji wa Sera ya Ajira ya Zanzibar ya mwaka 2009.
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana ambao wameshaanza kujiajiri wenyewe kutokana na mafunzo ya amali na ujasiriamali katika sehemu mbali mbali.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuwa zikisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa namna tofauti ikiwa ni pamoja na kuandaa sera na kutoa kauli mbiu katika vipindi tofauti.
Alisema kuwa kuna kauli mbiu zisemazo ‘kazi ni uhai’, ‘Uhuru na Kazi’, ‘Kazi ni Kipimo cha Utu’ na ‘Hapa Kazi tu’, kauli zote hizi si kwamba zinahamasisha watu kupenda kafanya kazi tu bali zina mantiki muhimu na pana katika ustawi wa maisha.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa katika kufanya kazi za maendeleo suala la uzalendo ni jambo la msingi kwani kunamjengea mtu hisia za kuamini kuwa anapaswa kuwajibika katika kuleta manufaa katika nchi na jamii yake.
Alisisitiza kuwa uzalendo ndio uliowaongoza waasisi wa Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 kujitoa muhanga kuikomboa Zanzibar ambapo pia, kutokana na kuwa na moyo wa uzalendo waaasisi hao na viongozi waliotangualia walishirikiana vyema na Serikali yao katika shughuli mbali mbali za ujenzi wa taifa kwa njia za kujitolea.
Aidha, alisema kuwa mafunzo mengine yanayopatikana kwenye utekelezaji wa Ibada ya Hijja ni kudhihirika kwa umoja na mshikamano wa Waislamu ulimwenguni kote.
Aliongeza kuwa jambo muhimu katika kuufikia umoja na mshikamano wa kweli ni kushirikiana na kuyaacha mambo yote yanayopelekea kufarakana na kuleta migogoro katika jamii ambapo kukosekana kwa umoja na ushirikiano ni kikwazo kikubwa cha kupata mafanikio.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ustahamilivu na uvumilivu ni mambo ya lazima ambayo binadaamu anapaswa ajipambe nayo huku akisisitiza kuwa ustahamilivu na uvumilivu si udhaifu bali ni miongoni mwa sifa za uongozi na utawala bora.
Post a Comment