Ads

Serikali kuboresha Huduma ya Uzazi wa Mpango kwa asilimia 45 kufikia mwaka 2020


Hussein Ndubikile, Mwambawahabari, Dar es Salaam
Serikali imesema kufikia mwaka 2020 malengo yake ni kuhakikisha asilimia 45 ya wanawake walioolewa wanatumia huduma za uzazi wa mpango huku ikibainisha kwa sasa asilimia 32 wanatumia huduma hizo lengo likiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akiwa na Ujumbe wa Waziri wa Maendeleo wa Uingereza, Penny Mordaunt auliotembelea katika Zahanati ya Tabata ‘A’ wilayani Ilala ili kuangalia huduma za uzazi wa mpango zinavyotolewa zahanati hapo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano kwa kushirikia na Serikali ya Uingereza imekuwa mstari mbele katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kupitia huduma hizo na kwamba lengo ni kupunguza vifo hivyo.

“  Waziri Penny amekuja kuangalia 
changamoto ya afya mama na mtoto na fedha wanazotoa tunazifanyia kazi inayokusudiwa kwani Serikali yetu na ya Uingereza zinashirikiana katika kuboresha huduma ya mama na mtoto,” amesema.

Amebainisha kuwa takwimu zinaonyesha wanawake 556,000 wanafariki kutokana na vifo vifo vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000.

Amesisitiza kuwa uzazi wa mpango unaweza kupunguza vitokananvyo na uzazi kwa asilimia 30 na kubainisha Serikali inaendelea kutenga rasilimali fedha za ndani kuboresha huduma za afya ikiwemo kuajiri watoa huduma za afya.

Kwa upande Waziri Penny amesema kuwa amefurahishwa alivyojionea huduma za uzazi wa mpango zinavyotolewa kwenye zahanati hiyo na kumpongeza Waziri Ummy kwa umahiri wa kusimamia utolewaji wa huduma hizo nchini hapa.

Akiwa katika Zahanati hiyo waziri huyo na ujumbe wake ametembelea Jengo la Kliniki ya Baba, Mama na Mtoto pamoja na Kikundi cha Umoja Group kinachojihusisha na Uzazi wa Mpango.

Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Zahanati ya Tabata ‘A’, Modest Mwinuka amesema zahanati Hiyo ni miongoni mwa vituo 88 vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto katika manispaa ya Ilala huku akisisitiza kati ya vituo hivyo, vituo 51 vinatoa huduma ya uzazi wa mpango.

Amesema zahanati hiyo inahudumia wakazi kutoka mitaa nane ikiwemo Tabata, Msimbazi, Tenge, Mandela, Mtambani, Msimbazi Magharibi,Matumbi pamoja na Tabata Kisiwani yenye wakazi74,742 kati yao wananume ni 18,593, wananwake 38,833 walio kwenye umri wa kuzaa ni 13,454.

“ Zahanati ina watumishi wapatao 29 wa kada mbalimbali wakiwemo waganga na wauguzi, kati yao 28 wamepatiwa mafunzo ya uzazi wa mpango, huduma rafiki kwa vijana, huduma baada ya mimba kuharibika na ukatili wa kijinsia,” amesema Mwinuka.

Mganga huyo ameongeza kuwa njia za huduma ya uzazi wa mpango zinazotolewa katika zahanati hiyo ni njia za muda mfupi ambazo ni vidonge, sindano, kondomu za kike na za kiume pamoja na njia ya shanga, njia ya muda mrefu(Kitanzi na vijiti), pamoja na nyingine za kudumu(kufunga kizazi mwanamke/mwanaume).

No comments