Tume Kuweka Bei Elekezi ya Madini
Na
Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
Serikali itapanga bei elekezi ya madini ili
kuwawezesha wachimbaji wadogo na wakubwa kunufaika na kazi yao.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini
Nchini, Prof. Idris Kikula akiwa katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za
uchimbaji wa madini Mkoani Dodoma.
Imebainika kuwa wachimbaji wa madini ya jasi
(Gypsum) wanalipwa fedha kidogo kwa tani moja kiasi kwamba gharama za
uzalishaji ni kubwa kuliko bei wanayopewa.
Mchimbaji wa madini katika kijiji cha Manda, Wilaya
ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, Saimon Msanjila amesema kuwa gharama ya uchimbaji
wa madini ya jasi tani moja na kuisafirisha hadi Dar es Salaam inafikia
Shilingi 65,000 na bei anayopewa ni Shilingi 77,000.
“Kwa kweli bei tunayopewa na wawekezaji wa viwanda
vya saruji ni ndogo sana, hivyo tunaiomba Serikali itusaidie katika hilo”,
alisema Msanjila.
Katika ziara hiyo wanakijiji cha Manzase, Wilayani
Chamwino walisimamisha msafara wa Tume ya Madini ili kueleze dukuduku lao kwa
uwekezaji unaoendelea katika eneo lao.
Hoja zao zilikuwa ni kumtaka mwekezaji atimize ahadi
yake ya kuwajengea daraja na kukarabati shule ya msingi.
Baada ya kuwasikiliza, Prof. Kikula alimtaka
mwekezaji huyo kufika kwenye ofisi ya madini kesho yake kwa hatua zaidi.
Wanakijiji wa Manzase na Manda kwa pamoja
waliishukuru Tume kwa kuwajali na kubaini changamoto walizonazo ili kuzipatia
ufumbuzi.
Aidha, Prof. Kikula amemtaka mwekezaji wa mawe ya nakishi kutangaza bidhaa zake
kwani zinaonekana zina ubora na zinafaa kwa ujenzi, hasa katika Makao Makuu.
Rai hiyo ameitoa katika kijiji cha Mapanga, Kata
ya Itiso, Wilayani Chamwino.
Kwa upande wake, Mwekezaji katika mgodi huo, Sisti
Mganga amesema soko la ndani ni dogo hivyo akaonyesha umuhimu wa kupata masoko
ya nje.
“Tunapanga kutafuta masoko nje na pia tutajenga
kiwanda cha kutengeneza mapambo ili tusipoteze chochote tunachochimba, na
tumepanga kuajiri watu wengi kwani kazi hii inahitaji nguvukazi kubwa”,alisema
Mganga.
Sisti amesema anaunga mkono juhudi za Rais John
Pombe Magufuli za ujenzi wa viwanda
Ziara hiyo ni endelevu kwani changamoto za
wachimbaji hasa wadogo ni nyingi na pia Serikali inataka ikusanye maduhuli yake
kupitia sekta ya madini.
Post a Comment