MAJALIWA AADHIMISHA SIKU YA MASHUJAA KWA KUSHIRIKI KATIKA KUFANYA USAFI WA MAZINGIRA ENEO LA COCO BEACH JIJINI DAR
Mwamba wa habari
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hali ya usafi Coco Beach hairidhishi na amewataka viongozi wa Manispaa
ya Kinondoni wajipange ili eneo hilo liweze kuvutia.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano,
Julai 25, 2018) wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kushiriki zoezi la
usafi wa eneo hilo pamoja na wananchi na watendaji mbalimbali ikiwa ni sehemu
ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa ambayo hufanyika Julai
25, kila mwaka.
Waziri Mkuu ambaye
aliambatana na mke wake, Mary Majaliwa, alishiriki zoezi hilo kwa kufyeka
nyasi, kuzoa takataka na kupanda miti kwenye ufukwe huo. Zoezi
hilo limefanyika kuanzia kwenye eneo la wafanyabiashara wa mihogo kuelekea Police
Officers’ Mess.
“Eneo hili nimelitembelea,
bado haliridhishi kwa usafi. Nimeenda kwenye fukwe pale na kukuta takataka nyingi
zimelundikwa mahali pamoja. Ni vema Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka zote
zinazosimamia usafi ziwaratibu wanaotoa huduma na wanaopata huduma ili kuendeleza usafi wa maeneo haya nchini kote,”
amesema.
Amesema Manispaa ya Kinondoni
haina budi kuratibu eneo hilo kwa kupanga eneo la maegesho, la watu kupumzikia,
la huduma za chakula na kuongeza kupanda miti ili wananchi waone ni maeneo
mazuri yanayovutia.
“Muandae shughuli za
burudani zitakazofanyika kila Jumamosi na Jumapili. Karibisheni watu wa kuleta
michezo ya baharini kama vile viboti na vibaiskeli vya majini, wekeni bembea
ili fukwe ivutie zaidi. Wazazi wataleta watoto wao kwenye michezo wakati wao wakikaa
pembeni na kupumzika,” amesema.
Amesema vibanda vilivyoko
kwenye ufukwe huo havipendezi na ikibidi waangalie uwezekano wa kuweka
makontena ili kuongeza mvuto. “Vibanda hivi havileti picha nzuri sana, hivyo
mnaweza kuweka makontena kutoka Pepsi au Coca-Cola ili kuleta muonekano sawia.”
“Jambo hilo linaweza kuwa ni
chanzo cha mapato kwa Manispaa hii. Uongozi wa Manispaa tengenezeni haya wakati
mkisubiri andiko lenu lipitishwe na muweze kupata fedha za kuboresha ufukwe
huu,” amesema.
Alisema eneo jingine linalopaswa
kuangaliwa katika ufukwe huo ni kuimarishwa kwa ulinzi ili watu wanaokwenda kupata
huduma wasihofie usalama wao.
Waziri Mkuu amesema usafi
siyo uishie kufanyika tarehe 25 tu, na akawataka watendaji wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa kwenye fukwe zote. “Hii ni changamoto kwenye Mamlaka ya
Halmashauri ya Kinondoni, lakini pia Ilala, Temeke, Bagamoyo hadi Tanga, zinapaswa
aihakikishe hizi fukwe ziwe safi,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kuzungumza na wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Ally Hapi alisema mbali
ya wananchi wa kawaida, walikuwepo pia askari polisi 100 na wanajeshi 150 ambao
walishiriki zoezi hilo la usafi.
Alisema Manispaa ya Kinondoni
wameanza kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu juu ya uboreshaji wa fukwe ya Coco
kwa kuandika andiko maalum na kulipeleka Ofisi ya Rais – TAMISEMI. “Manispaa
kupitia miradi ya kimkakati, tumeandaa andiko la kuomba sh. bilioni 11 za
kutengeneza na kuboresha ufukwe wa Coco, na tumeshalipeleka TAMISEMI na
mazungumzo yanaendelea,” alisema.
Juni
29 mwaka huu, wakati akitoa maelekezo kwenye hafla ya uzinduzi wa kituo cha
polisi kinachohamishika, Waziri Mkuu alisema: “Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli anawataka Watanzania wote waadhimishe siku hiyo ya kumbukumbu
ya mashujaa kwa kufanya usafi katika maeneo yaliyo jirani na makazi yao
pamoja na yale ambayo wamezikwa mashujaa ikiwa ni njia ya kuwaenzi.
Siku
hiyo hiyo, Waziri Mkuu alitangaza kwamba Rais Magufuli ameagiza kwamba sh.
milioni 308 zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Mashujaa, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Aliitaja
miundombinu hiyo ni pamoja na taa za kuongezea magari kwenye makutano ya barabara
ya Kisasa na barabara kuu ya Dodoma Dar es Salaam na kuweka taa za barabarani
kwenye barabara mpya ya mchepuko kutoka Emmaus hadi African Dream iliyojengwa ili
kupunguza msongamano wa magari yanayoingia kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JULAI
25, 2018.

Post a Comment