SERIKALI YATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA WA PAMBA YAFUTA DENI LA VIUADUDU.
NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
SERIKALI imefuta mikopo ya
wakulima ya viuadudu vyote vilivyotumika msimu huu katika zao la pamba nchini
na badala yake Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba utalipa madeni hayo.
Kauli hiyo imetolewa leo(jana)wilayani
Igunga na Waziri wa Kilimo Dkt . Charles
Tizeba wakati wa sherehe za uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba kwa mwaka
2018/19 ambapo kilo moja itanunuliwa kwa shilingi 1,100/-.
Alisema wakulima wa pamba ambao
wameshiriki katika kilimo cha mkataba watalipa mbegu na sio viuadudu ambazo
alikopeshwa na Kampuni mbalimbali.
Dkt. Tizeba aliongeza kuwa
wakulima ambao walinunua kwa kutumia fedha zao hatalipa chochote.
Aidha Waziri huyo aliongeza
kuwa katika msimu ujao wa kilimo wa 2019/20 hakutakuwepo na kilimo cha mkataba bali
Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la Pamba utaviwezesha vyama vya Ushirika vya
Msingi kupata pembejeo kwa ajili ya wakulima wote nchini.
Alisema wakulima watapatiwa
mbegu na viuadudu bure kulingana na uwezo wa mkulima kulima ili waweze kuongeza
uzalishaji wa zao hilo.
Aidha Dkt.Tizeba aliiagiza Bodi
ya Pamba nchini kushirikiana na Mahakama ili waweze kuwa na Mahakama
inayotembea(Mobile Court ) ili kudhibiti ubora na wizi kwa kutumia mizani.
Alisema AMCOS yoyote
iytakayobainika kuchezea mizani au kununua pamba chafu ichukuliwe hatua.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri aliwaonya viongozi wote wa Vyama vya Ushirika vya Msingi ambao
wamejiingiza katika uongozi kwa nia ya kuwaibia wakulima waondoke mara moja la
sivyo watakumbana na mkono wa Sheria.
Alisema hatakubali kuona
mkulima anaibiwa kwa kutumia mizani ya rula au kukata kilo na kuongeza kuwa
ushirika wa hivi sasa ni mahali patakatifu.
Mwanri aliongeza kuwa kiongoza
aliyepo madarakani ni lazima ajihakikishie kuwa yeye ni msafi na kama ana
rekodi ya wizi ni vema akaondoka mwenyewe kabla hayamkamata na kumweka ndani.
Alisisitiza kuwa hawezi
kusubiri wakulima waibiwe ndio hawakamate viongozi hata akisikia fununu za wizi
atalazima kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sharia.
Post a Comment