Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi Kupunguza Majanga Yatokanayo na Athari za Mabadiliko Hayo.
Mwambawahabari
Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma
Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa
Mataifa kuhusu mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi utainufaisha nchi kwa
kuimarika kwa Mipango ya Taifa ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi
ili kupunguza majanga yatokanayo na athari hizo.
Hayo yameelezwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba
wakati akiwasilisha Azimio la Bunge la kuridhia makubaliano ya mkataba huo.
"Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka
saini makubaliano hayo na hatimaye kuyatekeleza itanufaika na mambo mbalimbali
ikiwemo kuimarisha hali ya uchumi wa nchi na kujenga uchumi endelevu wa viwanda
wenye kustahimili mabadiliko ya tabianchi," alisema Mhe. Makamba.
Makamba Amesema, Mkataba huo utaongeza upatikanaji wa fursa
zilizopo za miradi na teknolojia safi itakayowezesha matumizi ya gesi asilia
majumbani na viwandani ili kuchochea maendeleo ya viwanda kwa kutumia nishati
yenye bei nafuu.
Vilevile, utaimarisha ushirikiano baina ya
Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa katika kusimamia na kutekeleza masuala
yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.
"Makubaliano ya Paris yanalenga kuboresha utekelezaji
wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 1992 kwa kutunza misitu inayonyonya joto, kuandaa na kutekeleza
mipango ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kuwa na mifumo ya upatikanaji wa
fedha na teknolojia safi kwa nchi zinazoendelea ili kukabiliana na changamoto
ya tabianchi," alifafanua Mhe. Makamba.
Aidha amesema, kwa kuzingatia manufaa yatokanayo
na Mkataba huo pamoja na itifaki yake kwa Tanzania na pia umuhimu na manufaa ya
makubaliano hayo, Bunge katika Mkutano wake wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa
Ibara ya 63 (3)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,
linaazimia kuridhia makubaliano ya Paris kuhusu kuboresha utekelezaji wa
Mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi yaani "THE PARIS AGREEMENT UNDER THE UN FRAMEWORK CONVENTIN ON CLIMATE CHANGE".
Post a Comment