TRA WAZINDUA UTOAJI WA VITAMBULISHO KWA WAFANYABIASHARA
Msajili wa Vitambulisho Dina Kaka akifafanua jambo leo jijini Dar es Salaam kuhusu utaratibu wa kupata vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Charles E. Kichere, akimkabidhi kitambulisho mfanyabiashara mdogo wa Soko la Kariakoo Bw. Mshamu Hassan.
Kitambulisho cha Mfanyabiashara mdogo
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles E. Kichere akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaaam kuhusu uzinduzi wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Sophia Mjema.
MWAMBA WA HABARI
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua utoaji wa Vitambulisho vya Wafanyabiashara wadogo ambao wapo kwenye Sekta isiyo rasmi wakiwemo wamachinga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaaam Kamishna Mkuu wa (TRA ) Charles Kichere, amesema kuwa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa wafanyabiashara wadogo itasaidia kufanikisha ulipaji wa kodi.
Amesema kuwa ili mfanyabiashara haweze kupata kitambulisho anatakiwa kujiunga katika vikundi maalum vinavyotambulika kisheria na serikali.
Bw. Kichere ameeleza mfanyabiashara huyo anapaswa kuwa na kitambulisho cha Taifa, namba ya utambulisho ya walipakodi ya kikundi alichojiunga pamoja na kuchangia Shillingi 10,000.
“Kitambulisho hicho kitamsaidia mfanyabiashara kutambulika katika taasisi za fedha na kupata mkopo ambao utakuwa msaada wa kukuza biashara yake” amesema Bw. Kichere.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema, amesema kuwa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho ni mfanikio makubwa kwani mpango huo ulikuwa unasubiriwa zaidi ya miaka miwili.
Amesema kuwa kufanikisha mpango wa vitambulisho sasa wamachinga watakuwa wanalipa kodi na kufanya kazi katika mazingira rafiki na kuwa tofauti na kipindi cha nyuma.
“Tutaendelea kushirikiana na wamachinga ili wafanya biashara zao na kutambulika na serikali bila kusumbuliwa na mtu yoyote” amesema Mhe. Mjema.
Utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara unatokana na marekebisho ya sheria ya usimamizi wa kodi ya mwaka 2015 yaliofanyiwa marekebisho na kikao cha Bunge la Bajeti mwaka wa fedha 2017/2018.
Miongoni mwa marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo ambao wapo katika sekta isiyokuwa rasmi.
Zoezi la hilo linatekelezwa na TRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (TIRA) pamoja na idara ya Uhamiaji.
TRA kwa kushirikiana na wadau wengine ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua Umoja wa Wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kuwapatia vitambulisho vya Taifa pamoja namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Hata hivyo imeelezwa kuwa vitambulisho hivyo vya wafanyabiashara vitadumu kwa muda wa miaka 3 ambapo vitakuwa na maelezo ya mfanyabiashara husika ikiwemo picha ya mfanyabiashara, jina la eneo analofanyia biashara, namba ya utambulisho wa mlipakodi na sahihi ya mfanyabiashara
Post a Comment