Ads

DIAMOND AKUTANA NA WAZIRI MWAKYEMBE NA SHONZA


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo Jumanne Machi 27mwaka huu amekutana na mwanamuziki Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz, jijini Dar es Salaam.

Tarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Lorietha Laurence imesema lengo la kukutana kwa wawili hao ni kurejesha maelewano kwenye tasnia ya muziki kufuatia hatua zinazochukuliwa na wizara hiyo kufungia baadhi ya nyimbo, zikiwemo mbili za mwanamuziki huyo.

Imeeleza kuwa katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za wizara hiyo na kuchukua zaidi ya saa tatu, kilihudhuriwa na naibu waziri wa wizara hiyo, Juliana Shonza, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mwingereza.

Wengine ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fisoo huku Diamond akifuata na mameneja wake watatu, Sallam Sharaff, Hamis Taletale na Said Fela.

Taarifa hiyo inaeleza mazungumzo hayo, Diamond alimhakikishia Dk Mwakyembe kushirikiana kwa karibu na Shonza na uongozi mzima wa wizara katika kusimamia maadili ya kazi za sanaa na kuwa mfano bora wa wasanii nchini katika kulinda utamaduni wa Tanzania.

Kwa upande wake Dk Mwakyembe amesisitiza kuwa Serikali haina ugomvi wowote na wasanii nchini bali ina tatizo na mmomonyoko wa maadili, kwamba kila msanii ana wajibu kulinda maadili ambayo ni sehemu ya utamaduni wa nchi.


“Mwakyembe alikumbushia kauli ya Mwalimu Julius Nyerere baada ya uhuru kwamba Taifa lisilo na utamaduni wake ni sawa na Taifa mfu na Watanzania kamwe tusigeuke Taifa mfu,” inaeleza taarifa hiyo ikimnukuu Dk Mwakyembe.

Waziri huyo ameagiza watendaji wa wizara na taasisi zake ikiwemo Basata, Bodi ya filamu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kukutana na makundi ya wasanii wa muziki kwa lengo la kuelimishana kuhusu taratibu za kuwasiliana na mamlaka husika za sanaa.

"Maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo yanayafanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa kiongozi wa wizara. Hivyo basi ieleweke kwamba hatua zilizochukuliwa na Shonza hivi karibuni zilikuwa za wizara kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema Dk Mwakyembe.

Kwa upande wake Shonza amesisitiza umuhimu wa wasanii kufuata utaratibu kwa kuwasilisha kazi zao mapema kwenye mamlaka husika iii kuepusha matatizo baadaye.

Lorietha Laurence Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo. 27/03/2018

No comments