MOI Wafanya Upasuaji Mwingine Mkubwa na Wa Kihistoria
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu upasuaji Mkubwa wa Nyonga uliofanya kwa
ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na Hospitali ya Prashanth Chennai
ya India
Madaktari Bingwa wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili kwa
kushirikiana na daktari bingwa wa
Mifupa kutoka hospitali ya Prashanth
Chenai ya nchini India leo wamefanya upasuaji mkubwa na mgumu wa kibingwa
wa kubadilisha kiungo cha nyonga (Complicated Total Hip Surgery) cha mgonjwa ambacho kimeharibika na
hivyo kumsababishia mgonjwa kushindwa kutembea na kupata maumivu
makali.
Upasuaji huo umefanywa na jopo la madaktari bingwa
wanne ambao wameongozwa na Dkt Mani Ramesh Kutoka India na Dkt Samweli
Kitugi Nungu wa MOI ambapo upasuaji huo umefanyika kwa ufanisi na
kwa masaa matatu.
Akizungumza baada ya Upasuaji huo Mkurugenzi Mtendaji
wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema ujio wa daktari kutoka India
ni sehemu ya mkakati wa Taasisi ya MOI kuwajengea uwezo wataalamu wake
kwa kupata mbinu mpya kutoka kwa wataalamu kutoka nchi mbalimbali.
Ushirikiano kama huu
“Mtaalamu huyu amekuwa hapa kwetu kwa siku tano,
naamini wataalamu wetu wamejifunza mbinu mpya za matibabu haya ya kibingwa
ya nyonga na lengo letu ni kuhakikisha hakuna mgonjwa anayekwenda nje
ya nchi kufuata matibabu ya aina hii. Pia, itasaidia kupunguza gharama
za mafunzo’’. Dkt Boniface
Pia, Dkt Boniface amesema kwa sasa Taasisi ya MOI
inawafanyia upasuaji wagonjwa 25-30 kwa mwezi idadi ambayo haijawahi
kufikiwa toka taasisi ianze kutoa huduma hizi za kibingwa za nyonga
mwaka 2003. Na malengo ni kufikia wagonjwa 100 kwa mwezi baada ya kuanza
kwa vyumba vipya viwili vya upasuaji katika jengo jipya la MOI (MOI
Phase III)
Kwa upande wake Dkt Mani Ramesh kutoka India amesema,
hii ni mara yake ya pili kufika MOI, amefarijika sana kwa namna Taasisi
ya MOI inavyotoa huduma zake kwa watanzania na pia ni shemu ya kubadilishana
uzoefu.
‘‘Nimefarijika sana kwa siku tano nilizokaa
hapa Tanzania, tumeshirikiana na kubadilishana uzoefu kwenye matibabu
haya ya kibingwa ya Nyonga, binafsi naamini huu ni muendelezo mzuri
wa ushirikiano kati ya MOI na hospitali yetu ya Prashant naamini nitarajea
tena hapa’’ Dkt Ramesh
Taasisi ya MOI imeshawafanyia upasuaji huu mkubwa
zaidi ya wagonjwa 1000 mpaka sasa na Taasisi inatarajia kufungua chumba
kipya cha upasuaji wa nyonga ambacho kitakuwa maalum kwa wagonjwa hawa
kwani mahitaji ni makubwa sana kwa sasa. MOI imeweza kufanikisha yote
haya kutokana na Serikali ya awamu ya Tano kutoa fedha za kununulia
vifaa tiba na kuboresha miundo mbinu kwa ajili ya kutolea huduma hizi.
Post a Comment