MAANDALIZI YA MFUMO WA PAMOJA WA KIELEKTRONIKI WA UONDOSHAJI SHEHENA YAANZA
Na Veronica Kazimoto,
Dar es Salaam
Serikali imeanza
maadalizi ya kutengeneza Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena
Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani kwa lengo la kuboresha
utendaji kazi na ufanisi.
Akizungumza leo Jijini
Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na
udhibiti wa mizigo katika maeneo hayo na wadau mbalimbali wa sekta binafsi, Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere amesema lengo la
kuwashirikisha wakuu hao ni kujenga uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa mfumo
huo.
“Uwepo wenu katika
mkutano huu ni muhimu sana kwasababu mtaweza kupitia mahitaji yote ya mfumo
yaliyoandaliwa na watalaamu wetu ikiwa ni pamoja na maeneo ya kisheria,
kiufundi na kibiashara ili muweze kuuboresha zaidi”, alisema Kichere.
Kichere alieleza
kuwa, uwepo wa wakuu hao na wadau wa sekta binafsi katika mkutano huo ni
kiashiria cha kuunga mkono adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga
mazingira bora ya kufanya biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Kamishna huyo Mkuu
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliongeza kuwa, Serikali imelenga kuwawezesha
wadau wote wanaohusika na biashara za kimataifa na usafirishaji wa mizigo
kutumia Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena kwa lengo la
kuwezesha uwasilishaji wa nyaraka mahali pamoja ili wadau wote waweze
kushughulikia nyaraka hizo kwa wakati.
Naye Mratibu wa Mfumo
wa Uondoshaji Shehena kutoka TRA Felix Tinka amezitaja faida za mfumo huo kuwa ni pamoja na kurahisisha na kuwezesha
biashara, kuongeza ufanisi wa matumizi bora ya rasilimali na kuongeza uhiari wa
ulipaji ushuru na tozo mbalimbali kwa waingizaji na waondoshaji wa mizigo.
“Mfumo huu una
faida nyingi, mbali na hizo nilizozitaja awali, pia kuna kuimarisha usalama,
kuimarisha uadilifu na uwazi katika utendaji kazi, kupunguza biashara haramu,
kupunguza gharama, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo katika vituo vya forodha
pamoja na kurahisisha ufuatiliaji wa mizigo kwa wakati”, Alisema Tinka.
Utekelezaji wa Mfumo
wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Bandarini, Viwanja vya Ndege
vya Kimataifa na Mipakani umegawanyika katika maeneo makuu matano ambayo ni
eneo la usimamizi wa mapato, uwezeshaji wa usafiri na uchukuzi, utekelezaji wa
sera na biashara, pamoja na usimamizi wa afya na usalama wa umma, usalama wa
uchumi pamoja na ugawaji.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Charles Kichere akizungumza leo jijini
Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na
udhibiti wa mizigo Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani
pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kuboresha utendaji
kazi na ufanisi. Pamoja nae ni Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA) Mussa Shilla.
Mwakilishi wa Mkemia Mkuu wa Serikali Daniel Ndiyo akichangia hoja leo jijini
Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Serikali wanaohusika na
udhibiti wa mizigo Bandarini, Viwanja vya Ndege vya Kimataifa na Mipakani
pamoja na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kwa lengo la kuboresha utendaji
kazi na ufanisi.
Post a Comment