WAFANYABIASHARA KIZIMBANI KWA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA
Na Mwandishi wetu.
Mume na mke ambao ni wafanyabiashara wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin gram 375.20.
Akisoma hati ya mashtaka leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini amewataja washtakiwa hao kuwa ni Minda Mfamai, mkewe Fatuma Mpondi na mwenzao Oswini Mango.
Wakili Mkini amedai Novemba 22, 2017 katika maeneo ya Chamazi kwa Mkongo Mbagala, wilayani Temeke, Dar es Salaam washtakiwa hao walisafirisha madawa hayo.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.
Hakimu Mashauri ameiarisha kesi hiyo hadi Desemba 19,2017 na kuamuru mshtakiwa Minda akatibiwe baada ya kulalamika kuwa alipigwa alipokuwa polisi.

Post a Comment