MWANAFUNZI MBARONI KWA KUKUTWA NA SARE ZA JWTZ
Lazaro Mambosasa akiwa na sare za JWTZ alizokutwa
nazo mwanafunzi
MWAMBA WA HABARI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam,linamshikilia
mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Fahari iliyopo Goba Said
Selemani (17) kwa kosa la kukutwa na sare za JWTZ (Kombat).
Mwanafunzi huyo alikamatwa maeneo ya Mbezi CRDB
bank akiwa amevaa sare hizo za JWTZ huku akivuta sigara hadharani na kufanya
vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare.
Akizungmza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, SACP Lazaro Mambosasa amesema
katika mahojiano ya awali kijana huyo alijitambulisha ni askari kutoka kikosi
cha 501 KJ kilichopo Lugalo jijini humo.
"Baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata sare
hizo kutoka kwa rafiki zake anaokuwa nao sehemu mbalimbali,"amesema.
Amesema alipopekuliwa katika begi la mgongoni
alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja pamoja na kitambulisho namba DFF
7001A cha familia ya askari chenye namba 1231 ambacho ni cha mtoto wa askari wa
JWTZ MT 65640 Private Gabriel Kihwili wa 501 KJ kikiwa na
picha ya mtoto wake Elia Gabriel.
"Uchunguzi bado unaendelea ili kuwapata rafiki
zake hao ambao inadhaniwa kuwa huwa wanashirikiana katika kufanya matukio ya
kihalifu,"amesema.
Katika hatua nyingine,jeshi hilo lilifanikiwa
kuwakamata watuhumiwa watatu waliokuwa wakijihusisha na matukio ya uporaji na
mauaji mbalimbali jijini humo wakiwa na silaha aina ya AK. 47 na risasi 57.
"Baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikubali
kuonesha silaha moja aina ya AK.47, Magazine mbili (2) na risasi 57 ambayo
walikuwa wameificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano.
"Pia walionesha pikipiki mbili aina ya Boxer
zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE rangi
nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali,"amesema.
Amesema walipohojiwa walisema wanazo silaha
nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda
kuonyesha silaha hizo.
"Walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari
jambazi mmoja raia wa Burundi aliyefahamika kwa jina la Fanuel Luchunda
Kamana alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha huku wenzake wawili
wakijaribu kutoroka na ndipo walijeruhiwa kwa risasi,"amesema.
Mambosasa amesema majambazi hao waliwahishwa katika
hospitali ya Mwananyamala ili kupatiwa matibabu na ndipo madaktari wakabaini
kuwa tayari wameshafariki dunia.
Amefafanua kuwa miili imehifadhiwa hospitalini hapo
kwa hatua za uchunguzi wa kitaalamu.
Amesema awali majambazi hao walikiri kufanya
matukio kadhaa ya uporaji na mauaji likiwemo tukio la mauaji huko Kunduchi
Mtongani lililotokea Novemba /2017 ambapo uuwa madereva bodaboda na kupora
pikipiki zao na kuziuza kwa sh.800, 000.
"Majambazi wengine waliofariki ni Gallus
Marandu Clement (31) na Fredrick Wilbroad Achalo mkazi wa
Gongo la Mboto,"amesema.
Ameongeza kuwa Novemba 11/2017 jeshi hilo
walikamata gari aina ya Ipsum lenye namba T. 142 CNF na radio call aina ya
motorola maeneo ya Mbezi Msumi pamoja na kamba za katani na vipande viwili vya
nondo vilivyokuwa vikitumiwa na kundi la majambazi wapatao watano waliokuwa
wamevamia katika nyumba ya Erick Mkwemwa.
"Awali majambazi hao wapatao watano walifika
katika nyumba hiyo na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa Polisi waliofika
hapo kwa ajili ya kufanya upekuzi lakini badala yake waliwaweka chini ya ulinzi
familia hiyo na kuwafunga kamba mikononi,miguuni kisha kuwaziba na plasta
mdomoni na hatimaye majirani wa eneo hilo walitilia mashaka kitendo hicho na
kuamua kuizingira nyumba hiyo huku wakitoa upepo matairi ya gari,"amesema.
Amesema majambazi hao walipobaini kitendo hicho
walianza kukimbia huku wakifukuzwa na wananchi ambapo wawili kati yao
walikamatwa na kuanza kushambuliwa kwa kupigwa fimbo/mawe na hatimaye
walifariki dunia huku wengine watatu wakifanikiwa kutoroka.
"Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika
hospitali ya taifa ya Muhimbili huku msako mkali ukiendelea ili kuwakamata
majambazi wengine 3 waliokimbia,"amesema.
Ameongeza kuwa, jeshi hilo lilifanikiwa kumuuwa
jambazi sugu aliyetumia bastola feki(Iliyotengenezwa kienyeji) katika kupora
pikipiki mwenye umri Kati ya miaka 25-30.
"Awali jambazi huyo alimkodi dereva pikipiki
ili ampeleke maeneo ya Msitu wa Jeshi huko Buza lakini ghafla walipofika maeneo
hayo jambazi huyo alitoa bastola yake iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na baruti
na kumuamuru dereva ashuke na kumuachia pikipiki,baada ya kushuka dereva
alipiga kelele kuomba msaada na ndipo wananchi walijitokeza na kuanza kumpiga
kwa mawe huku wengine wakimkata mapanga,"amesema.
Amesema askari walipata taarifa na walipofika eneo
hilo walimkuta jambazi huyo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake
na ndipo walimkimbiza katika hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu na
muda mfupi baadae alifariki dunia.
Ameeleza kuwa jeshi hilo lilikamata bajaji yenye
namba za usajili MC 473 BMM rangi ya blue iliyoibwa Kigamboni Mjimwema nyumbani
kwa Chandra Kandri.
"Baada ya askari kupata taarifa ya kupotea kwa
bajaji hiyo ufuatiliaji ulianza mara moja na ndipo Bajaji hiyo ilipatikana huko
Sumbawanga mkoani Rukwa ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana baada ya
kushindwa kufanya zoezi la kubadilisha umiliki wake,"amesema.

Post a Comment