NAIBU WAZIRI WA KILIMO MARY MWANJELA: AWATAKA WAFANYABIASHARA KUUZA MBOLEA KWA BEI ELEKEZI
Mwambawahabari
Na Mathias Canal, Mbeya

Makatibu tawala kote nchini wametakiwa
kutafiti na kubaini wafanyabiashara wadogo wa mbolea wanaokiuka bei
elekezi kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuwauzia wafanyabiashara hao
wadogo kwa bei elekezi ya rejereja badala ya bei ya jumla.
Mwito huo umetolewa na Naibu
Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa wakati akihutubia kwenye
ufunguzi wa mkutano wa kwanza kati ya mikutano saba (7) katika Kanda
saba (7) za kilimo nchini inayotegemewa kufanyika ambao ni muhimu kwa
makatibu tawala na washauri wa kilimo wa mikoa ya nyanda za juu kusini
wa kuelimishana kuhusu ubora wa mbolea na mfumo wa bei elekezi ambao
umefunguliwa rasmi.
Mhe Naibu Waziri wa Kilimo
aliwasihi Makatibu Tawala hao wa Mikoa na wataalamu wa kilimo
kuhakikisha kwamba wanasimamia bei elekezi ya mbolea, Wanatoa Elimu kwa
Wakulima ili wanunue mbolea bora na pia kuimarisha vikundi vya wakulima
ili waweze kutumia nguvu ya umoja katika kuboresha kilimo kwa ajili ya
utoshelevu wa mahitaji ya kaya zao na kuuza ziada hapa nchini na nchi za
nje.
Alisema kuwa wafanyabiashara
licha ya kufahamu kuwa wanatakiwa kugawana faida na wauzaji wa rejareja
lakini bado wanakiuka taratibu za kisheria hivyo aliwaagiza kuacha tabia
hiyo ili mawakala wauze kwa rejareja na kwa bei elekezi bila kuathiri
biashara zao.
Alisema Katika Sekta ya
Kilimo mbolea ni moja ya pembejeo zinazohitaji ushirikiano mkubwa
kutokana na ukweli kwamba inahitajika kwa wingi na ina gharama kubwa,
inahitaji utaalamu katika matumizi yake na kwamba ni bidhaa
inayoharibika kwa haraka endapo viwango vya utunzaji wake havizingatiwi.
Mhe Mwanjelwa aliwaagiza
wakaguzi wote wa mbolea nchini kufuatilia na kuhakikisha kwamba kila
mfanyabiashara wa mbolea ana leseni ya kufanya biashara ya mbolea ambayo
itatolewa bure na TFRA na pia wahakikishe kwamba wote wamepata mafunzo
haraka iwezekanavyo.
“Mbolea ni moja ya
vichocheo vikubwa sana katika suala hili na hivyo, mwisho wa mkutano huu
tunategemea kupata taarifa ya mikakati ya namna Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa zitakavyosimamia ubora na bei elekezi ya mbolea ili
Mkulima aweze kuipata na kuitumia kwa lengo linalokusudiwa,” alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Naibu Waziri huyo alisema
kuwa Wizara ya kilimo ilitunga Kanuni ya Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja
(Fertilizer Bulk Procurement Regulations) na kuzitangaza kwenye Gazeti
la Serikali kupitia tangazo G.N. 49/2017. Pamoja na kuunda kanuni hizo,
Wizara ya kilimo ilirekebisha Kanuni ya Mbolea ya mwaka 2011 kwa Kanuni
zilizotangazwa katika Gazeti la Serikali kwa tangazo G.N. Na. 50/2017
ili kuipa nguvu TFRA kukokotoa, kutangaza na kusimamia bei elekezi ya
mbolea.
Aliwaagiza pia
wafanyabiashara wanaotunza mbolea bila kuzingatia viwango vilivyowekwa
na TFRA kuacha haraka tabia hiyo kwani kwani wanasababisha mbolea
kumfikia mkulima ikiwa imepungua ubora au kuharibika kabisa na hivyo
kumfanya mkulima asipate tija inayotokana na matumizi ya mbolea.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe
Mary Mwanjelwa amewataka wataalamu hao Kutenda haki katika uwajibikaji
wao, Kufanya kazi kwa weledi, uaminifu, uwajibikaji uliotukuka, na
nidhamu ya hali ya juu.
Aliongeza kuwa kwa yeyote
atakaye kwenda kinyume na matakwa ya serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt
John Pombe Magufuli itamchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Post a Comment