Ads

UPELELEZI KESI YA LEMA WAKAMILIKA.

UPELELEZI wa kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, dhidi ya Rais John Pombe Magufuli, umekamilika. 


Hata hivyo, Mahakama ya Wilaya ya Arusha, iliahirisha kusikiliza maelezo ya awali hadi Oktoba 24, itakaposikilizwa mbele ya Hakimu Devotha Msofe, kutokana na mbunge huyo kutokuwapo mahakamani jana. 

Lema ambaye kwa sasa yupo Nairobi akimuuguza mbunge mwenzake Tundu Lissu, anadaiwa kufanya uchochezi dhidi ya Rais Magufuli. 

Akiomba kuahirishwa kwa kesi hizo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Jasmine Abdul, Wakili wa Serikali, 
Fortunatus Mhalila, aliiambia mahakama kuwa kesi hizo zilikuja kwa ajili ya Lema kusomewa maelezo ya awali ya mashtaka yanayomkabili, lakini kwa kuwa yupo nchini Kenya aliomba ipangwe tarehe nyingine. 

Awali Mei 29, mwaka huu, Hakimu Mkazi Desdery Kamugisha, aliyekuwa akisikiliza kesi hizo alijitoa kuendelea kusikiliza kesi namba 
441/2016. 

Katika kesi hiyo, Lema anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii, Oktoba 23, mwaka jana, katika mkutano wa hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa. 

Lema anadaiwa kutamka, “Kiburi cha Rais kisipojirekebisha…Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake. 

“Rais ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu 
wananyanyaswa.” Lema alinukuliwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Martenus Marandu. 

Katika kesi nyingine, ilidaiwa kuwa Lema anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi Oktoba 22, mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara. 

Miongoni mwa maneno anayodaiwa Lema kutoa ni kuwa: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani, iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu…“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya Katiba, Rais huyo ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua, wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.” 

Lema alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Kamugisha Novemba 8, mwaka jana, akikabiliwa na kesi hizo  na Novemba 11, mwaka jana, alishindwa kupata dhamana baada ya Mawakili wa Serikali kuwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufani Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ya kupinga uamuzi wa dhamana uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. 

Lema alikaa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi minne, kutokana na kukosa dhamana katika kesi hizo kuanzia Novemba 11, mwaka jana kabla ya kuachiwa kwa dhamana Machi 3, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

No comments