Ads

KUBENEA AUGUA GHAFLA.

MBUNGE wa Ubungo mkoani Dar es Salaam, Saed Kubenea (Chadema) ameshindwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge baada ya hali yake kuwa mbaya kiafya, akipelekwa mbele ya kamati hiyo na askari Polisi akiwa katika baiskeli ya kusukuma wagonjwa. 

Mbunge huyo alipewa muda wa kupata huduma ya kwanza katika Zahanati ya Bunge mjini hapa jana. Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Newala, George Mkuchika (CCM), iliridhia kwamba asihojiwe hadi hapo baadaye. 

“Kutokana na hali yake na maombi yake mwenyewe kuomba tumpe muda ili aendelee kupata matibabu, kamati imeridhia ombi hilo,” alisema Mkuchika na kuongeza kuwa kamati imekubali maombi yake na imeagiza mara moja apelekwe Zahanati ya Bunge na apatiwe huduma ya kwanza, na kisha atachagua mahali pa kwenda kupata matibabu. Alisema Kubenea alisafirishwa kwenda mkoani Dodoma, kufikishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka kuhojiwa baada ya kupelekewa wito wa kufika mbele ya kamati hiyo. 

Alisema Kubenea aliitwa mbele ya kamati hiyo kutokana na kudharau Mamlaka ya Spika katika kauli ambazo alizitoa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima jijini Dar es Salaam. Mkuchika alisema ukitakiwa kufika mbele ya kamati unapelekewa hati ya kuitwa, hivyo Kubenea alishapelekewa hivyo alifika. “Siku moja tukakubaliana kufanya kikao hicho saa tisa alishindwa kufika sababu alilazwa katika Kituo cha Afya Bungeni,” alieleza Mkuchika. Alisema baada ya hapo, walisubiri ndipo Spika aliamuru apelekwe na Polisi.

No comments