Ads

Okwi: Mbao sio watu wamchezo mchezo.

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.

STRAIKA wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema hakuweza kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Mbao FC, kwani mabeki wa wapinzani wao hao walimkamia kupita kiasi. 

Okwi hakuweza kufurukuta dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa juzi Alhamisi kwani alitulizwa kwa kuchezewa rafu mara 12. 

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao iliilazimisha Simba sare ya mabao 2-2 na kuwa timu ya kwanza kutikisa nyavu za Wekundu wa Msimbazi msimu huu. 

Okwi, mwenye mabao sita katika ligi kuu akiwa kinara wa ufungaji, alishindwa kufunga kutokana na mabeki wa Mbao kuwa makini wakiongozwa na Boniface Maganga na Yusuph Mgeta. 

Kwa pamoja na wachezaji wengine wa Mbao, mabeki hao walimchezea Okwi raia wa Uganda faulo 12 katika muda wote wa dakika 90 za mchezo huo. 

Akizungumza baada ya mchezo huo, Okwi alisema Mbao walimkamia kupita kiasi ndiyo maana alishindwa kufunga: “Mbao walikamia sana aisee kwani mabeki wao walikuwa wakinikaba hadi kivuli. 

“Nilijitahidi kutumia mbinu zangu lakini imekuwa ngumu kweli lakini tunashukuru Mungu kwa sare hii kwani tangu msimu uliopita nilisikia Mbao inaisumbua sana Simba.” 

Hata hivyo, mwamuzi aliyechezesha mchezo huo, Athuman Lazi aliwapa kadi za njano baadhi ya wachezaji wa Mbao kwa kucheza mchezo usiofaa kwa wachezaji wa Simba akiwemo Okwi.

No comments